
Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Clinton amesema kuwa, hakuna uadilifu katika mfumo wa vyombo vya sheriria vya nchi hiyo.
Clinton ambaye anatazamiwa kugombea nafasi ya urais katika uchaguzi wa mwaka 2016 nchini Marekani, ameyasema hayo alipokuwa akiashiria tukio la mauaji ya kijana mwenye asili ya Afrika Michael Brown aliyeuawa kwa kupigwa risasi na afisa wa polisi huko mjini Ferguson, Missouri na kuongeza kuwa, serikali inaweza kuchukua hatua kali kukabiliana na tukio hilo na mengineyo kama hayo.
Akizungumzia maandamano ya hivi karibuni ya kupinga mauaji na ukandamizaji uliokithiri dhidi ya jamii ya Wamarekani weusi nchini humo, amesema kuwa, serikali haitakiwi kufumbia macho mapungufu na vitendo vinavyokinzana na uadilifu katika idara za mahakama nchini.
Ameitaka serikali kufanya juhudi kubwa kurejesha hali ya uaminifu wa wananchi kwa serikali.
Siku chache zilizopita miji mbambali ya Marekani hususan Ferguson, ilishuhudia wimbi la maandamano makubwa, ya kupinga ubaguzi wa rangi na ukatili vinavyofanywa na polisi wa nchi hiyo dhidi ya Wamarekani wenye asili ya Kiafrika.
Kufuatia tukio hilo Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Navi Pillay, aliitaka Marekani kujiangalia yenyewe kabla ya kuzituhumu nchi nyingine za dunia kuwa zinakiuka haki za binaadamu.