Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF) umetangaza kuwa kuna uwezekano wa kushuka chini kiwango cha ustawi wa kiuchumi katika nchi zilizokumbwa na virusi vya homa ya Ebola.
Kwa sasa nchi za Sierra Leone, Liberia na Guinea zimeathiriwa sana na ugonjwa huo hatari.
Msemaji wa IMF
Gerry Rice amesema kuwa shirika hilo linashirikiana na nchi hizo tatu kwa ajili ya kutayarisha ripoti ya awali juu ya taathira mbaya za kiuchumi za mgogoro wa Ebola na kiwango cha bajeti inayohitajika kwa ajili ya kuzisaidia nchi hizo.
Sierra Leone, Liberia na Guinea ni miongoni mwa nchi zinazopokea mkopo wa Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF) katika mpango wa muda mrefu wa kuzisaidia nchi maskini.
Mbali na nchi hizo tatu, virusi vya Ebola pia vimeripotiwa katika nchi za Nigeria, Senegal na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Mkurugenzi wa Mpango wa Chakula Duniani (WFP) kanda ya Afrika magharibi Denise Brown alitangaza hivi karibuni baada ya kuzitembelea nchi za Liberia na Sierra Leone kwamba juhudi za kusitisha wimbi la kuenea virusi vya Ebola katika nchi za magharibi mwa Afrika ni sawa na kuogelea katikati ya mawimbi ya tsunami.
Brown ambaye aliandamana na mratibu wa Umoja wa Mataifa kuhusu virusi vya Ebola amesema, Mpango wa Chakula Duniani kamwe haujawahi kukumbana na mgogoro mkubwa wa aina hii.
Amesema jamii ya kimataifa inajua njia za kukabiliana na migogoro ya zilzala, machafuko ya vita na mawimbi ya tsunami lakini inaonekana kwamba imeshindwa kupambana na ugonjwa huo unaoenea kwa kasi kubwa.
Mkurugenzi wa WFP katika eneo la magharibi mwa Afrika ameongeza kuwa kuna ulazima wa kufanyika jitihada za pamoja kupitia njia ya anga, kutoa zana na vitendea kazi, mifuko ya kubebea maiti, na misaada ya chakula na kwamba watu wote wanapaswa kuelewa umuhimu wa mapambano hayo.
Virusi vya homa ya Ebola vilifumuka mwanzoni mwa mwaka huu katika nchi ya Guinea Conakry na baadaye vikaenea katika nchi za Sierra Leone, Liberia na Nigeria.
Inasemekena kuwa maambukizi ya sasa ya virusi hivyo ndiyo mabaya zaidi tangu Ebola igunduliwe mwaka 1976 katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Ripoti zinasema kuwa watu wasiopungua 1500 wamepoteza maisha kutokana na mfumuko wa sasa wa ugonjwa huo.
Vilevile kuwepo kwa kesi zinazodhaniwa kuwa za homa ya Ebola katika nchi za Uhispania na Ubelgiji kunazidisha wasiwasi juu ya kasi ya kuenea ugonjwa huo katika maeneo mbalimbali duniani.
Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuwa kuna uwezekano Ebola ikawaathiri maelfu ya watu na kwamba linatekeleza statijia ya kukabiliana na kasi ya kuenea zaidi virusi hivyo katika maeneo yaliyoathiriwa.
