Israel imesema kuwa ina mpango wa
kunyakua mamia ya hekta za ardhi katika eneo ililolighusubu la Ukingo wa
Magharibi wa Mto Jordan.
Vyombo vya habari vya utawala wa Kizayuni wa
Israel vimetangaza kuwa, mpango huo ni sehemu ya miradi ya Tel Aviv ya
kuendeleza ujenzi wa vitongoji vya walowezi. Duru za jeshi la Israel
zimeripoti kuwa hekta za ardhi karibu ya 400 katika kitongoji cha Gevaot
kusini mwa mji wa Bait-laham zimetangazwa kuwa ni ardhi ya Israel.
Wakati huo huo baraza la vitongoji la
Israel limekaribisha mpango huo mpya wa kupanua makazi ya walowezi wa
Kizayuni na kueleza kuwa mradi huo utafungua njia ya kupanuliwa
kitongoji cha Gevaot na pia kuanzisha mji mpya.
Taasisi isiyo ya
kiserikali ya Israel kwa jina la B'Tselem imeeleza kuwa Tel Aviv imepora
mamia ya maelfu ya hekta za ardhi kutoka kwa Wapalestina huko katika
Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan tangu mwaka 1967 kwa minajili ya
kujenga vitongoji zaidi ya 200 vya walowezi wa Kizayuni.