Vikosi vya usalama vya Somalia
vimezima shambulio la wanamgambo wa al Shabab katika makao makuu ya
masuala ya kiintelijinsia na kitengo cha mahabusu huko Mogadishu mji
mkuu wa nchi hiyo.
Polisi na watu walioshuhudia wameeleza kuwa shambulio
hilo la leo lilianza baada ya kulipuka gari lililokuwa limetegwa bomu
nje ya kituo cha taifa cha masuala ya intelijinsia, mlipuko uliofuatiwa
na shambulio la watu wenye silaha waliovalia sare za jeshi la taifa la
Somalia.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya
Somalia amesema kuwa mmoja wa wavamizi ameuawa kwenye mlipuko wa bomu na
wengine sita wameuliwa na vikosi vya usalama.
Msemaji wa Wizara ya
Mambo ya Ndani ya Somalia ameongeza kuwa shambulio hilo limekwisha na
kwamba wavamizi wameshindwa kutimiza lengo lao la kuvuruga oparesheni ya
bahari ya Hindi akiashiria oparesheni ya nchi kavu inayotekelezwa sasa
na Umoja wa Afrika na serikali ya Somalia.
Wakati huo huo Msemaji wa
kundi la al Shabab Abdulaziz Abu Musab amethitibitisha shambulio hilo na
kudai kuwa wanamgambo wao wamewaua maafisa kumi wa usalama na kuwaachia
huru mahabusu kadhaa.