JESHI LAMUONDOA MADARAKANI WAZIRI MKUU LESOTHO

 
  Waziri Mkuu wa Lesotho aondolewa madarakani na jeshi
 
Waziri Mkuu wa Lesotho Thomas Thabane ameondolewa madarakani na jeshi. 
 
Thabane ambaye kwa sasa amekimbilia nchi jirani ya Afrika Kusini, amesema kuwa kitendo hicho cha kuondolewa madarakani kilichotekelezwa na jeshi la nchi hiyo hapo jana kinakinzana na matakwa ya wananchi. 
 
Thomas Thabane pia alikitaja kitendo hicho kuwa ni aina fulani ya mapinduzi ya kijeshi.
 
 Kwa mujibu wa ripoti, mapema jana milio ya risasi ilisikika  Maseru, mji mkuu wa nchi hiyo ndogo ya kifalme inayozungukwa na Afrika Kusini, ambapo vikosi vya jeshi vilichukua udhibiti wa makao makuu ya polisi na kuzingira nyumba ya Waziri Mkuu.
 
 Inaelezwa kuwa kamanda mkuu wa jeshi la nchi hiyo alikuwa anakusudia kumtia mbaroni waziri mkuu huyo na naibu wake na kuwakabidhi kwa mfalme.
 
 Hii ni katika hali ambayo wakati Thomas Thabane anayataja matukio ya hivi karibuni kuwa ni mapinduzi ya kijeshi, msemaji wa jeshi la nchi hiyo kwa upande wake, mbali na kukadhibisha habari za kutokea mapinduzi ya kijeshi ametangaza kuwa, hatua ya kuvinyang'anya silaha vikosi vya polisi, ilikuwa ni kwa minajili ya kuzuia umwagikaji damu na machafuko ambavyo vingeweza kutokea ndani ya nchi hiyo.
 
 Pamoja na hayo hivi karibuni Waziri wa Michezo wa Lesotho, Thesele Maseribane mbali na kutangaza kudhibitiwa makao makuu ya jeshi la polisi, alielezea pia kuwepo uwezekano mkubwa wa kutokea mapinduzi ya kijeshi nchini humo.
 
 Hayo yanajiri katika hali ambayo hatua ya hapo awali ya kugawana madaraka na kuundwa baraza la mawaziri kwa ushiriki wa vyama mbalimbali, ilileta matumaini ya kupatikana maendeleo na ustawi ndani ya nyoyo za raia.
 
 Karibu miaka miwili iliyopita, baada ya chama cha Waziri Mkuu wa Lesotho cha All Basotho Convention (ABC) kuungana na baadhi ya vyama vya upinzani, kilifanikiwa kutwaa uongozi wa taifa hilo.
 
 Awali Lesotho ilikuwa ikiongozwa na waziri mkuu wa zamani, Pakalitha Mosisili aliyeongoza nchi hiyo kwa miaka 14 na ambaye alikuwa mwanachama wa chama tawala cha wakati huo cha Kongresi ya Kidemokrasia. Katika uchaguzi uliopita, Mosisili hakufanikiwa kutwaa ushindi wa kura nyingi, huku chama chake kikipata viti 40 kati ya viti vyote 80 katika bunge la taifa. 
 
Wakati huo huo pia baadhi ya vyama vya siasa vikakataa kujiunga na chama cha Kongresi ya Kidemokrasia. Suala ambalo lilifungua uwanja wa kuingia madarakani Thomas Thabane.
 
 Thabane aliunda chama chake cha All Basotho Convention (ABC) "Basotho" hapo mwaka mwaka 2006, ambacho ni tawi lililomeguka kutoka chama cha Kongresi ya Lesotho kwa ajili ya Demokrasia. 
 
Muda mchache baadaye chama chake kiligeuka kuwa chama kikubwa mashuhuri cha upinzani dhidi ya serikali iliyokuwa madarakani wakati huo.
 
 Kwa kutumia udhaifu wa Mosisili, Thabane akafanikiwa kujiongezea mapenzi ya wananchi. Mosisili alikuwa akituhumiwa kuwa anawapa nyadhifa muhimu serikalini watu wa kabila lake na hivyo kuonekana mtu mwenye ukabila.
 
 Mbali na hilo, umasikini uliokithiri katika kipindi cha utawala wake, ulipelekea kuongezeka manung’uniko ya wananchi dhidi ya kiongozi huyo.
 
 Ni wakati huo huo ndipo jina la Thabane likapata umashuhuri kufuatia kaulimbiu yake ya kupambana na umasikini na kuinua uchumi wa Lesotho.
 
 Hatimaye sambamba na kupata ushindi wa viti 26 katika bunge, akafanikiwa pia kupata nafasi ya pili katika uchaguzi.
 
 Muungano wa vyama viwili vya upinzani vya Kongresi ya Lesotho kwa ajili Demokrasia na chama cha Kitaifa cha Basotho, uliandaa mafanikio ya Thabane na hivyo kupelekea kupata viti vingi bungeni na hivyo ikawa sababu ya yeye kutakiwa aunde serikali.
 
 Pamoja na hayo tangu awali baadhi ya weledi wa mambo waliuhisi muungano wa vyama hivyo kuwa ni wenye kusuasua.
 
 Hivi sasa kuondolewa madarakani Waziri Mkuu wa nchi hiyo, kumepunguza sana kiwango cha matarajio juu ya kustawi demokrasia ndani ya nchi hiyo ya kusini mwa Afrika.