Machafuko nchini Cameroon yamekuwa yakichukua mkondo mpya siku hadi siku. Ripoti zinaonyesha kuwa vitendo vya utumiaji silaha na mabavu vimekuwa vikiongezeka kaskazini mwa nchi hiyo ya Kiafrika. Viongozi wa Cameroon wamekuwa wakijaribu kuonyesha kuwa vitendo hivyo vinatekelezwa na wanamgambo wa Boko Haram walio na ngome kuu yao katika nchi jirani ya Nigeria, jambo ambalo linatiliwa shaka na wataalamu wa mambo. Uwezekano wa vitendo vya ugaidi au njama za kisiasa kuvuruga hali ya usalama huko Cameroon umezusha wasiwasi mkubwa nchini humo. Wachambuzi wengi wa masuala ya kisiasa hawafutilii mbali uwezekano wa kuzuka wimbi la upinzani na uasi dhidi ya Rais Paul Biya wa nchi hiyo. Ni wazi kuwa mawaziri na viongozi wa zamani wa Cameroon wanamtaka Biya ang'atuke madarakani. Rais Paul Biya aliye na umri wa mika 81 amekuwa akitawala nchi hiyo kwa miaka 32 sasa. Vyombo vya habari na hasa magazeti ya nchi hiyo yamekuwa yakiripoti visa vya kuongezeka ghasia na machafuko yanayodaiwa kuchochewa na Boko Haram kaskazini mwa nchi hiyo, katika mpaka wake na Nigeria. Eneo hilo kwa miezi kadhaa sasa limekuwa likishuhudia ongezeko kubwa la mashambulio ya umwagaji damu yanayodaiwa kutekelezwa na magenge ya Boko Haram. Jina la Boko Haram kwa mara ya kwanza lilianza kusikika huko Cameroon mwezi Februari 2013 kufuatia kutekwa nyara nchini humo kwa familia moja ya Kifaransa. Hofu na woga kuhusiana na kundi hilo ulitanda hata zaidi kufuatia kundi hilo kutangaza mnamo Oktoba 2013 kuwa lilikuwa limemteka nyara kasisi mwingine wa kigeni.
Pamoja na hayo lakini kuachwa nyuma kwa silaha zilizotengenezwa huko Israel zilizotumiwa na watekajinyara katika shughuli hiyo kuliacha shaka kubwa katika fikra za waliowengi. Silaha hizo hutumiwa tu na askari wa kikosi cha radiamali ya haraka pamoja na walinzi wa rais wa Cameroon. Mwei Aprili, kambi ya wafanyakazi wa Uchina nchini Cameroon ilivamiwa na magari mengi kuibiwa katika tukio hilo. Kufuatia tukio hilo mkuu wa Baraza la Kitaifa la Cameroon alionya kuwa kulikuwa na maadui ambao walikuwa wameazimia kuvuruga usalama na kuzusha ghasia nchini humo.
Kwa vyovyote vile vita vya kuwania madaraka nchini Cameroon vimepamba moto na wanasiasa wengi wa nchi hiyo wanaona kuwa wanafaa kuhudumia nafasi ya rais wa nchi. Wakati huohuo umasikini mkubwa uliokita mizizi katika maeneo ya kaskazini mwa Cameroon umetoa mwanya wa kununuliwa vijana wasio na kazi ili wajiunge na makundi yanayobeba silaha kwa maslahi ya wanasiasa. Ubaguzi mkubwa unaofanyika katika nchi hiyo ni jambo jingine ambalo linawakera sana wananchi. Maeneo ya kaskazini yanahisi kuwa yanabaguliwa kwa misingi ya kikabila na kusahaulika kabisa na serikali kuu ya Cameroon. Hii ni kutokana na ukweli kuwa Rais Biya ameweka karibu yake na kuwapa nyadhifa muhimu za serikali watu wa kabila lake ambao kimsingi wanatoka kusini mwa nchi. Mbali na suala la ubaguzi, tuhuma za kufanyika udanganyifu katika uchaguzi wa 2011 ni jambo jingine linalohatarisha msingi wa utawala wa Biya. Pamoja na hayo yote lakini baadhi ya wajuzi wa mambo wanasema kuwa itakuwa vigumu kumg'oa madarakani Rais Biya kutokana na kuwa ana ushirikiano mkubwa na serikali ya Ufaransa.