
Kuendelea mapigano na hali ya mchafuko nchini Libya mbali na kusababisha matatizo ya kiusalama, kumeifanya nchi hiyo kwa sasa ikabiliwe na tatizo jingine ambalo ni la raia kuwa wakimbizi.
Duru za Libya zimeripoti kwamba, kuna ongezeko kubwa la wimbi la wakimbizi na raia wa nchi hiyo wanaoomba hifadhi katika nchi za jirani.
Takwimu zilizotolewa na viongozi wa Libya zinaonesha kwamba, kutokana na kuendelea mapigano baina ya pande mbili hasimu katika mji mkuu Tripoli, takribani familia elfu hamsini mjini humo zimelazimika kuyakimbia makazi yao.
Hivi karibuni Umoja wa Mataifa ulitangaza katika ripoti yake kwamba, karibu raia milioni moja nchini Libya wamelazimika kuwa wakimbizi ikiwa ni natija ya kuendelea nchi hiyo kugubikwa na machafuko.
Baadhi ya wakimbizi hao wameelekea katika nchi za jirani huku baadhi yao wakielekea Ulaya na kukubali kuhatarisha maisha yao kutokana na kutumia njia ya baharini.
Msemaji wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR amewaambia waandishi wa habari kwamba, takribani watu elfu thelathini na saba kutoka miji ya Tripoli na Benghazi wamejisajili katika ofisi ya shirika hilo ambapo akthari yao ni wale ambao wanaishi katika maeneo ambayo yanakabiliwa na mapigano kati ya makundi hasimu ya Libya.
Kwa mujibu wa UNHCR ni kuwa, tangu ulipoanza mwaka huu, Walibya elfu sabini na saba wamekimbilia Italia kupitia njia ya baharini.
Takwimu hizo zinatolewa katika hali ambayo, duru za habari kwa upande wake zinaripoti juu ya kuibuka wimbi jipya la wakimbizi wa Libya wanaoelekea katika nchi za Misri na Tunisia.
Baadhi ya nchi jirani na Libya ikiwemo Tunisia zimefunga mipaka yao na Libya na hivyo kuwafanya wakimbizi kutoka Libya watangatange mpakani wasijue waelekee wapi.
Katika mazingira kama haya, Jumuiya ya Hilali Nyekundu na Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu yamesisitiza kwamba, endapo vurugu na machafuko yataendelea nchini Libvya, basi raia milioni mbili wa nchi hiyo watakabiliwa na hatari ya uhaba wa chakula.
Katika upande mwingine, Umoja wa Mataifa umetoa indhari kuhusiana na hali ya Libya na kutangaza kwamba, nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika inakabiliwa na hali ya kusikitisha ambayo inaelekea katika mkondo mbaya zaidi.
Katika hali ya hivi sasa baadhi ya mashirika ya misaada yameondoka nchini Libya kutokana na hofu ya kukabiliwa na mashambulio ya wanamgambo au ya jeshi la nchi hiyo, hatua ambayo kivitendo imeifanya hali ya Libya kuwa tata zaidi.
Hivi karibuni nchi jirani na Libya ziliitisha mkutano ambao ulijadili masuala ya nchi hiyo na namna ya kumsaidia jirani yao huyo ili ajinasue kutoka katika kinamasi alichonasa.
Wapembuzi wa mambo wanaamini kwamba, mkutano huo unabainisha wasi wasi walionao majirani wa Libya kutokana na kukosekana usalama katika nchi hiyo.
Machafuko na ukosefu wa usalama nchini Libya umekabiliwa na radiamali mbalimbali kimataifa. Baadhi ya nchi za Magharibi ikiwemo
Marekani zimeanza kuzungumzia udharura wa kutumia nguvu za kijeshi kukabiliana na hali ya sasa ya nchi hiyo.
Hata hivyo Jumuiya ya Nchi za Kiarabu imesema kuwa, haiungi mkono uingiliaji wa kigeni katika matukio ya sasa ya Libya.
Pamoja na hayo viongozi wa Libya sanjari na kuitaka jamii ya kimataifa iwasaidie katika matatizo wanayokabiliwa nayo, wamezitaka pande zinazopigana nchini humo kuachana na machafuko na badala yake zitumie njia za mazungumzo ya kisiasa kwa shabaha ya kutatua matatizo yaliyopo na hivyo kuruhusu nchi hiyo iende katika mkondo wake wa kukamilisha mchakato wa kisiasa.