Shirika moja la kimataifa linaloshiriki katika mpango wa kulijenga upya
eneo la Ukanda wa Gaza baada ya mashambulio ya kinyama ya utawala wa
Kizayuni wa Israel limetangaza kuwa unahitajika muda wa miaka 20 kwa
ajili ya kulikarabati eneo hilo.
Shirika la Shelter Cluster ambalo
linaendeshwa kwa pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia
Wakimbizi UNHCR na mashirika ya Msalaba Mwekundu na Hilali Nyekundu
limeripoti kuwa, katika mashambulio ya utawala wa Kizayuni dhidi ya
Gaza, jumla ya nyumba elfu 17 zilibomolewa au kuharibiwa vibaya na
nyengine elfu tano ziliharibiwa kwa kiwango kidogo cha kuhitajia
matengenezo.
Shirika la Shelter Cluster limeongeza kuwa makadirio ya
muda wa ukarabati yanategemea uwezo wa vivuko vikuu vya kupitishia vifaa
vilivyoko baina ya Gaza na ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu
ambapo makadirio yaliyofanywa ni kupitishwa kila siku malori mia moja ya
vifaa vya ujenzi kuelekea Gaza.
Wakati huo huo Umoja wa Mataifa
umetangaza kuwa hivi sasa eneo la Ukanda wa Gaza lina uhaba wa nyumba
elfu 75 za kuishi.
Ikumbukwe kuwa mbali na Wapalestina wapatao 2,150
waliouliwa shahidi, katika mashambulio ya kinyama ya utawala wa Kizayuni
dhidi ya Gaza yaliyoanza tarehe 8 Julai hadi 26 Agosti maelfu ya
nyumba, zaidi ya misikiti 80, zaidi ya shule 140 na majengo 350 ya
viwanda na karakhana yalibomolewa…/