
ZIPO taarifa kwamba Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF imewaita Yanga na Mchezaji wao kutoka Uganda, Emmanuel Okwi, ili kuzungumza sakata lake kufuatia Simba kumchukua Mchezaji huyo ambae ana Mkataba na Yanga.
Kamati hiyo ya TFF inatarajiwa kukutana Septemba 6 na hatua hii imekuja mara tu baada ya Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji, kuitaka TFF kulishughulikia suala la Mchezaji huyo ndani ya Siku 7 na pia kumtaka Okwi kuilipa Yanga Dola 500,000 kwa kukiuka Mkataba wake.
Inaaminika Okwi ana Mkataba wa Miaka Miwili na Nusu na Yanga lakini Juzi Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Pope, alimtangaza kama Mchezaji mpya wa Simba.
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa TFF, Celestina Mwesigwa, alisema kuwa wao bado wanamtambua Okwi kama bado ni Mchezaji wa Yanga na hawajapata taarifa yeyote rasmi kuwa Mchezaji huyo amehama.
Habari toka Simba zimedai Jina la Okwi limepelekwa TFF kama mmoja wa Wachezaji Watano wa Kigeni wanaoruhusiwa kucheza Ligi Kuu Vodacom.
Wageni wengine wa Simba ni Joseph Owino kutoka Uganda, Wachezaji wawili wa Burundi, Pierre Kwizera na Amisi Tambwe, na Mchezaji wa Kenya Paul Kiongera.