Wanafunzi 700 shule tatu za msingi Bunda hoi kwa madarasa, wanafunzi wakalia magogo na mawe kujisomea

Hali hiyo imeelezwa kuwa chanzo kikuu cha kudhoofisha hali ya taaluma katika wilaya hiyo kwa kiwango kikubwa.
Taarifa zilizoifikia FikraPevu Agosti 31, 2014 zinaeleza kuwa licha ya wanafunzi hao kukaa chini wakati wa masomo pia shule hizo zina matundu machache ya choo, ikiwemo matundu manne ya shule ya msingi Machimweru yanayotumiwa na wanafunzi pamoja na Walimu 18 wa shule hiyo.

“Shule nyingi hapa wilayani Bunda zinakabiliwa na uhaba wa madawati, vyoo, matangi kwa ajili ya kukingia maji ya mvua, na bajeti ndogo kwa ajili ya kukarabati miundombinu ya shule kwa maana tumekuwa tukiwaambia madiwani wakifanya mikutano na wananchi wahamasishe suala la kuchangia miundombinu hii lakini zoezi hili limeshindwa kufanikiwa kwa muda mrefu,” anasema.

Hata hivyo, amesema matokeo ya miaka miwili iliyopita kuanzia mwaka 2012 shule hiyo ilikuwa ya 79 kati ya shule 155 zilizofanya mtihani wa darasa la saba na mwaka 2013 ilishika nafasi ya 139 kati ya shule 158 na kuwa tatizo la mimba kwa wanafunzi shuleni bado ni changamoto.
Amesema ofisi ya Mkurugenzi wa
Halmashauri ya wilaya ya Bunda kushirikiana na Idara ya Elimu ya Msingi
na Sekondari wameanza kuzunguka katika shule hizo na kuhamasisha walimu
kujituma katika kuongeza kiwango cha ufaulu mashuleni.
Imeelezwa kuwa takribani wanafunzi 130 wa shule ya msingi Kinyambwiga A wanasoma wakiwa chini ya miti ambayo imegeuzwa kama vyumba vya madarasa na kuwa wanafunzi hao ni wa darasa la pili na darasa la tano, ambapo wameiambia FikraPevu iliyowatembelea shuleni hapo kuwa wanahitaji serikali iwatatulie kero hiyo ili kuboresha kiwango cha elimu shuleni hapo.
Wamesema wanaathirika kiafya na kielimu kutokana na mazingira wanayosomea na kuwa wakati mvua zikinyesha hulazimika kujibanza kwenye madarasa machache ya shule hiyo yaliyo na unafuu katika miundombinu ya majengo.

Afisa Elimu wa Shule za Msingi wa Wilaya ya Bunda, Jeshi Pembe, alithibitisha wanafunzi hao kujisomea katika mazingira hayo na kuwa, hali hiyo inasababishwa na wananchi wa vijiji hivyo kutokuwa na utayari wa kuchangia nguvu zao kwa ajili ya kushirikiana na serikali kwa ajili ya kujenga vyumba vya madarasa na kutengeneza madawati.
Aidha, imebainika kuwa shule nyingi zilizopo wilayani humo hazina miundombinu rafiki kwa wanafunzi na kupelekea baadhi ya wazazi na walezi kutotilia umakini suala la kusomesha watoto hususani watoto wa kike ambapo wengi wao huolewa wakiwa na umri mdogo kwa kukatisha masomo.

Uchumi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda unatokana na kilimo, madini, mifugo na uvuvi, shule za Wilaya hiyo kamwe haziwezi kukosa vyumba vya madarasa, madawati, nyumba za walimu na nyingine kufungwa kwa kukosa matundu ya vyoo.

Imeelezwa kuwa baadhi ya wazazi wamekata tamaa kwa ajili ya kuchangia shughuli za ujenzi wa shule za msingi katika wilaya hiyo kutokana kushindwa kutoa michango ya kuendeleza miundombinu ya shule kwa kukosa kipato hata cha kuhudumia familia zao.
Katika tukio la hivi karibuni lilioripotiwa na FikraPevu ilibainika kuwa wanafunzi wengi katika Wilaya ya Butiama walikatisha masomo kutokana na tatizo la mimba.
CHANO; FikraPevu