Serikali ya Somalia jana
iliwasilisha malalamiko kwa Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu, kwa ajili
ya kutatua hitilafu zilizopo kati yake na Kenya.
Viongozi wa Somalia
wametaka kuanishwa kwa makini mipaka ya baharini kati ya nchi hiyo na
Kenya.
Mjadala uliopo sasa kati ya nchi mbili
hizo juu ya haki ya kuchimba mafuta na mapato yanayotokana na maliasili
hiyo katika maeneo yenye mafuta kwenye mipaka ya majini, umezidisha
wasiwasi wa kuibuka mapigano.
Kwa mujibu wa barua ilitowasilishwa na
Somalia katika Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu, mazungumzo
yaliyofanywa na nchi mbili hizo hadi sasa yameshindwa kutatua hitilafu
zilizopo.
Hitilafu za mpaka kati ya Somalia na
Kenya si suala jipya.
Nchi mbili hizo kwa miaka kadhaa sasa zimekuwa
zikivutana kuhusu akiba ya mafuta katika bahari ya Hindi.
Hitilafu kati
ya Kenya na Somalia pia zimeyaathiri makampuni ya mafuta ya nchi kadhaa
yanayoendesha shughuli zao katika eneo la mashariki mwa Afrika.
Weledi wa mambo wanaamini kuwa, katika
hali ambayo Somalia inakabiliwa na tatizo la maharamia, mchafuko ya
ndani, vitisho vya kundi la al Shabab, jeshi dhaifu na uwezekano wa
kutokea tena janga la njaa nchini humo, vita kati ya nchi hiyo na
majirani zake, ni changamoto mpya ambayo inaweza kuyafanya maisha ya
raia wa Somalia kuwa magumu zaidi.
Pamoja na hayo yote na licha ya
kuweko matatizo ya aina mbalimbali, wapembuzi wa mambo wanasema hatua
yoyote ya kusalimu amri serikali ya Mogadishu mbele ya haki zake katika
maji ya Bahari ya Hindi inakinzana na maslahi ya nchi hiyo.
Hasa
ikitiliwa maanani kwamba, madola makubwa ya eneo hilo na yale ya mbali
yamepanga mikakati ya kuwa na udhibiti katika maji ya bahari hiyo
kutokana na kuweko maliasili muhimu hususan maliasili na akiba ya
nishati jadidika katika Bahari ya Hindi.
Bahari ya Hindi ni bahari ya tatu kwa
ukubwa duniani. Bahari hiyo ni pia mlango la kuingilia bahari saba
muhimu za dunia na milango bahari minne ya kistratejia yaani Hormoz,
Babul Mandan, Malaka na Suez.
Zaidi ya asilimia 40 ya biashara ya
kimataifa inapita katika mlango bahari wa Malaka na asilimia 40 ya
mafuta ghafi yanayozalishwa duniani hupitia katika mlango bahari wa
Hormoz.
Wakati huo huo asilimia 60 ya bidhaa na biashara ya kimataifa
hufanyika kupitia Bahari ya Hindi.
Imeelezwa kuwa, hadi kufikia mwaka
2030, mahitaji ya nishati ya dunia yataongezeka kwa asilimia 45.
Usafirishaji wa asilimia 70 ya mafuta
duniani kupitia Bahari ya Hindi ni ishara ya umuhimu wa bahari hiyo
katika suala la nishati duniani.
Weledi wa mambo wanaamini kuwa, kupenda
makuu na tabia ya kujitanua ya baadhi ya nchi vinavuruga na kuharibu
mazingira ya ushirikiano.
Vilevile ni wazi kuwa miongoni mwa sababu
muhimu za kuwepo ustawi katika nchi za kanda hiyo ni kujiepusha na
mizozo na hitilafu.
Kwani kuwepo hitilafu na mgawanyiko kutayapa madola
ya kikoloni fursa ya kuingia tena katika eneo hilo na kupora maliasili
zake.
Kwa msingi huo ilitarajiwa kwamba nchi
jirani za Kenya na Somalia zilipaswa kuketi chini na kutafuta suluhisho
la amani la mgogoro wa mpaka wa majini na hivyo kuzuia uwezekano wa aina
yoyote wa kuyapa fursa madola ya kikoloni.