Duru za jeshi la Cameroon zimeripoti
kuwa, zaidi ya wanajeshi 20 wa nchi hiyo wameuawa katika kipindi cha
mwezi mmoja uliopita katika vita dhidi ya wanamgambo wa Boko Haram.
Duru
hizo zimetangaza kuwa, wanajeshi 25 wa Cameroon wameuawa katika kipindi
cha mwezi mmoja kufuatia mapigano ya jeshi la nchi hiyo na kundi la
wanamgambo wa Boko Haram wenye makao yao nchini Nigeria.
Taarifa zaidi
zinasema kuwa, wanajeshi hao wameuawa katika mapigano huko kaskazini mwa
Cameroon ambapo kunashuhudiwa kuongezeka mashambulio ya Boko Haram.
Katika miezi ya hivi karibuni, jeshi la
Cameroon limeanzisha vikosi vipya na kutuma vikosi vya kuongeza nguvu
katika maeneo ya kaskazini mwa nchi hiyo kwa shabaha ya kupambana na
wanamgambo wa Boko Haram wanaoripotiwa kuendesha operesheni za
mashambulio katika maeneo hayo.
Pamoja na hayo serikali ya Cameroon
inalaumiwa na wapinzani na wananchi wengi wa nchi hiyo kutokana na
kushindwa kukabiliana na wanamgambo wa Boko Haram.