Watu wawili wameuawa katika mji mkuu wa Somalia Mogadishu, baada ya wanamgambo wa al-Shabab kulishambulia kwa risasi gari la afisa mmoja wa serikali.
kijuzi.blogspot.com
Ripoti zinasema kuwa, wanachama wanne wa al-Shabab waliokuwa katika gari la kifakhari wamelishambulia kwa risasi gari la Ali Mohamed Madobe katika Wilaya ya Wadajir mjini Mogadishu.
Mohamed Hassan, mmoja wa maafisa usalama mjini Mogadishu ameziambia duru za habari kwamba, gari la afisa huyo wa serikali lilishambuliwa akiwa njiani kuelekea ofisini kwake na kwamba, waliouawa katika shambulio hilo ni mlinzi na dereva wake.
Aidha Ali Mohamed Madobe mwenyewe amejeruhiwa vibaya katika shambulio hilo.
Sheikh Abdiasis Abu Mus’ab msemaji wa al-Shabab amethibitisha kwamba, kundi lao ndilo lililotekeleza shambulio hilo.
Tangu aliyekuwa kiongozi wa al-Shabab Ahmad Abdi Godane auawe mwanzoni mwa mwezi huu, maafisa usalama wa Somalia wamejiweka tayari kukabiliana na mashambulio tarajiwa ya wanachama wa kundi hilo ya kulipiza kisasi cha kuuawa kiongozi wao.
Wanamgambo wa al-Shabab wametangaza wazi kuwa, watalipiza kisasi cha kuuawa Godane na kwamba, inaratibu mashambulio pia dhidi ya Marekani ambayo ndiyo iliyohusika na mauaji ya kiongozi wao huyo.