Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei amesema Hija ni fursa muhimu ya kufaidika umma wa Kiislamu na rehma za kimaanawi katika ardhi ya wahyi na kuimarisha uhusiano wao na Mwenyezi Mungu.
Ayatullah Khamenei ameyasema hayo leo katika mkutano na maafisa wanaosimamia msafara wa Hija ya mwaka huu na kubainisha kwamba msimu wa Hija ni fursa adhimu ya kurekebisha masuala ya kidini na kimaanawi pamoja na masuala muhimu ya Ulimwengu wa Kiislamu.
Ameongeza kuwa katika masiku ya Hija Waislamu wanapaswa kuzitumia kikamilifu fadhila za kimaanawi za safari hiyo na kuimarisha uhusiano wao na Mwenyezi Mungu kwa namna itakayopelekea kushuhudiwa mabadiliko ya kweli baada ya safari ya Hija.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumzia pia utumiaji wa fursa ya Hija kwa ajili ya kuchunguza masuala muhimu ya Ulimwengu wa Kiislamu na kubadilishana mawazo kwa lengo la kutatua matatizo na akafafanua kwamba leo hii Ulimwengu wa Kiislamu uko katika mazingira tete mno ambapo moja ya masuala muhimu zaidi yanayoukabili ni njama na mbinu za madola ya kibeberu za kuchochea hitilafu na kudhaniana vibaya Waislamu.
Sanjari na kusisitiza kwamba katika masiku ya Hija inapasa kutumia uwezo wote uliopo na kujitahidi kusafisha nyoyo na kuondoa chuki za kupandikizwa, Ayatullah Khamenei amesema: kwa masikitiko, na kutokana na kujisahau, baadhi ya Waislamu wa Kishia na Kisuni wanazushiana tuhuma na uongo na hivyo kuwasaidia maadui wa Umma wa Kiislamu na kutumikia maslahi ya Marekani na Uzayuni.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema ukufurishaji katika mazingira ya sasa ni miongoni mwa silaha na nyenzo zinazotumiwa na maadui wa Uislamu kuchochea hitilafu baina ya Waislamu na kuwashughulisha wao kwa wao ili kuwaghafilisha na suala la Palestina na badala yake kuhudumia maslahi ya utawala wa Kizayuni; na akasisitiza kwamba suala la Palestina ndilo suala la kwanza la Ulimwengu wa Kiislamu ambalo linapasa kuzingatiwa na kupewa umuhimu katika Hija…/