BALOZI WA KUDUMU WA SYRIA AWKOSOA WAUNGAJI MKONO WA DAESH

Al-Jaafari awakosoa waungaji mkono wa Daesh
Balozi na mwakilishi wa kudumu wa Syria katika Umoja wa Mataifa amewakosoa waungaji mkono wa kundi la kigaidi na Daesh na kusema kuwa, Saudi Arabia, Uturuki na Qatar ndiyo waungaji mkono wakuu wa kundi hilo la kigaidi katika Mashariki ya Kati. 

Bashar al-Jaafari amesema hayo katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kubainisha kuwa, hatua yoyote ile dhidi ya magaidi inapaswa kuchukuliwa kwa misingi ya sheria za kimataifa. Al-Ja’afari amebainisha kuwa, katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, serikali ya Damascus imepigana kiume dhidi ya magaidi.
Mwakilishi wa kudumu wa Syria katika Umoja wa Mataifa ameashiria ushirikiano na uratibu baina ya serikali ya nchi hiyo na Iraq katika vita dhidi ya ugaidi na kusema kuwa, vita nchini Syria na Iraq dhidi ya ugaidi ni vita moja dhidi ya adui mmoja. Amesisitiza kwamba, nchi zote mbili zimekuwa waathiriwa wa ugaidi mmoja.