MAZUNGUMZO; Waasi na serikali ya Mali waanza tena mazungumzo


  Waasi na serikali ya Mali waanza tena mazungumzo

Duru ya pili ya mazungumzo ya amani kati ya serikali ya Mali na makundi yanayobeba silaha ya kaskazini mwa nchi hiyo imeanza nchini Algeria.

 Imeelezwa kuwa lengo la duru hii ya mazungumzo ni kujaribu kurejesha amani na utulivu katika maeneo yanayosumbuliwa na machafuko kaskazini mwa Mali.

 Awamu ya kwanza ya mazungumzo hayo ilifanyika tarehe 4 Julai katika mji mkuu wa Algeria, Algiers ambapo pande mbili zilitia saini ramani ya njia ya mazungumzo kati yao.

 Modibo Keita waziri mkuu wa zamani wa Mali na mwakilishi wa Rais wa nchi hiyo katika mazungumzo ya serikali ya Bamako na makundi ya waasi hivi karibuni alisisitiza kwamba, katika mazungumzo ya awamu hii pande mbili zitajadili masuala ya ndani zaidi na kwamba, ana matumaini duru hii ya mazungumzo itakamilika kwa pande husika kutia saini hati ya makubaliano ya amani.

 Serikali ya Mali imekuwa ikikabiliwa na mgogoro wa kisiasa tangu Januari mwaka 2012 baada ya makundi yenye silaha ya Tuareg kuanzisha mashambulio katika maeneo ya kaskazini mwa nchi hiyo.