Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS imesema matamshi yaliyotolewa na Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina dhidi ya harakati hiyo hayana msingi wowote.

Msemaji wa HAMAS Sami Abu Zuhri amesema karibuni hivi yatafanyika mazungumzo kati ya wawakilishi wa harakati za HAMAS na Fat’h kuhusu hati ya makubaliano ya maridhiano ya kitaifa ya Palestina yaliyosainiwa mwezi Aprili mwaka huu.
Inafaa kuashiria kuwa wakati alipowasili mji mkuu wa Misri, Cairo hapo jana usiku, Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina aliituhumu HAMAS kuwa inakwamisha kuanza kufanya kazi serikali ya maridhiano ya kitaifa na kushika hatamu za mamlaka katika Ukanda wa Gaza na kutishia atakata mashirikiano yake na harakati hiyo.
Amedai kwamba HAMAS inaendesha serikali kivuli huko Gaza na kwamba anachotaka yeye ni kuwepo mamlaka moja na mfumo mmoja tu wa utawala.
Itakumbukwa kuwa kufuatia makubaliano ya maridhiano ya kitaifa yaliyotiwa saini tarehe 23 Aprili kati ya harakati za Fat’h na HAMAS, tarehe pili Juni Mahmoud Abbas alitangaza huko Ramallah kuundwa serikali ya maridhiano ya kitaifa ya Palestina…/