Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haina hamu ya kushiriki katika mkutano wa kimataifa uliopangwa kufanyika wiki ijayo mjini Paris Ufaransa kwa madhumuni ya kupambana na kundi la kitakfiri la Daesh (ISIL) linalotenda jinai na mauaji katika nchi za Iraq na Syria.
Hayo yameelezwa leo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayeshughulikia masuala ya nchi za Kiarabu na za Afrika, Hussein Amir- Abdullahian ambaye ameongeza kuwa mkutano huo una orodha ya wageni wa kuchaguliwa na unafanyika kimaonyesho tu
Amesema kuhudhuria katika mkutano wa kimaonyesho wa kupambana na ugaidi huko Paris hakumo katika ajenda ya Iran.
Amefafanua kuwa Iran inafadhilisha kile alichoeleza kuwa ni “vita vya kweli na si vya kuchagua” vya kupambana na ugaidi katika eneo na ulimwenguni kwa jumla.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amekumbusha kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilikuwa nchi ya kwanza iliyochukua hatua haraka ya kuisaidia Iraq kupambana na ugaidi na kusisitiza kwamba Tehran itaendelea kutoa uungaji mkono mkubwa na wa adhati kwa Iraq na Syria katika kupambana na ugaidi.
Wakati huohuo Kamanda wa Jeshi la Kujitolea nchini la Basij amesema Ikulu ya Marekani White House ndio makao makuu ya kundi la kitakfiri la Daesh (ISIL).
Brigedia Jenerali Mohammad Reza Naqdi amesema Washington ndiyo iliyoliunda kundi hilo kwa malengo mawili; la kwanza likiwa ni kuchafua na kuharibu sura ya Uislamu kwa kuvionyesha kupitia vyombo vya habari duniani vitendo vya kinyama na jinai za kutisha zinazofanywa na kundi hilo. Naqdi amesema lengo la pili la Marekani ni kuleta mpasuko, uadui na vita kati ya Waislamu wa Kishia na Kisuni.
Kamanda wa Jeshi la Kujitolea la Basij amewataka Waislamu wote kudumisha umoja na kuepuka masuala yanayochochea migogoro ya kidini…/