
Phiri alimpanga beki Isihaka Rajabu katika mechi ya kirafiki dhidi ya Gor Mahia akicheza katika nafasi ya Donald Mosoti na alimudu vyema na kuitendea haki nafasi hiyo.
Kutokana na uwezo aliouonyesha beki huyo katika mchezo huo, Phiri ameamua kumkabidhi majukumu yote yaliyokuwa yanafanya na Mosoti katika ukuta huo wa ulinzi.
Akizungumza hivi karibuni Jijini Dar es Salaam wakati wa mazoezi wa Timu yake, Phiri alisema Mchezaji huyo ni mzuri na anaamini kuwa anamudu vema nafasi hiyo licha ya kuwa bado kuna makosa kidogo anahitaji kuyarekebisha.
Alisema licha ya kuwa Mosoti ni Beki mzuri lakini anaamini kuwa Wachezaji hao wataweza kufanya vizuri katika nafasi hiyo na kufanikiwa kuliziba kabisa pengo la Mosoti aliyeachwa na Simba.
Simba inatarajiwa kuanza kutupa karata yake ya kwanza kesho katika michuano ya Ligi Kuu Bara, huku ikiwa na sura za Wachezaji 13 wageni waliojiunga na kikosi hicho msimu huu.
Wachezaji hao ni Pierre Kwizera, Peter Manyika, Hussein Sharif, Abdi Banda, Elius Maguli, Paul Kiongera, Shaaban Kigisa, Joram Mgeveke, Isihaka Rajabu, Mohamedi Hussein, Abdul Makame, Ibrahimu Ajibu na Adam Miraji.