
Hakimu wa mahakama moja ya Afghanistan leo ametoa hukumu ya kifo kwa watu saba baada ya kupatikana na hatia ya kuwabaka kwa pamoja wanawake wanne katika kesi iliyoamsha moto wa hasira nchi nzima huku umati wa watu wenye ghadhabu ukiwa umekusanyika nje ya mahakama hiyo wakati kikao cha kesi hiyo kilipokuwa kikirushwa hewani moja kwa moja kupitia televisheni.
Katika hukumu waliyosomewa, wanaume hao saba wamepatikana na hatia ya kuwateka nyara na kuwashambulia wanawake waliokuwa kwenye kundi la msafara wa magari yaliyokuwa yakitoka harusini na kuelekea mji mkuu wa nchi hiyo Kabul.
Katika kesi hiyo iliyochukuwa muda wa saa chache tu mahakama ilielezwa kwamba katika tukio lililojiri tarehe 23 ya mwezi uliopita wa Agosti, watu hao, huku wakiwa wamevalia sare za polisi na kubeba bunduki waliusimamisha msafara wa magari, wakawaburuza wanawake wanne kutoka ndani ya gari hizo, wakawapora vito vya thamani, wakawapiga na kisha wakawabaka.
Imeripotiwa kuwa mmoja wa wanawake hao alikuwa mmoja mzito.
Mapema Rais Hamid Karzai alitoa wito wa kutaka watu hao wanyongwe. Naye Mkuu wa Polisi ya Kabul Zahir Zahir ametilia mkazo wito huo na kusema wanataka watu hao wanyongwe hadharani ili liwe funzo kwa wengine…/