Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa
taarifa iliyotolewa na Baraza la Ushirikiano wa Ghuba ya Uajemi (GCC)
kuhusu visiwa vitatu vya Iran vya Tombu Kubwa, Tombu Ndogo na Abu Mussa
inaonesha jinsi nchi wanachama wa baraza hilo zisivyoelewa uhakika wa
historia na hali ya sasa ya eneo hili.
Bi Marziyeh Afkham amesema, taarifa hiyo ni kielelezo cha
wazi cha kuingilia mambo ya ndani ya Iran na kwamba Tehran mbali na
kulaani taarifa hiyo inasisitiza kuwa, misimamo kama hiyo haina faida
yoyote na inapotosha fikra za watu na kuchelewesha ushirikiano wenye
faida kati ya nchi za Ghuba ya Uajemi.
Mwishoni mwa mkutano wao wa Jumamosi iliyopita huko Jiddah,
Saudia Arabia, Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi za GCC walitoa taarifa
wakidai kuwa visiwa hivyo vitatu yaani Tombu Kubwa, Tombu Ndogo na Abu
Mussa si milki ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran
. Katika vikao vyake vya
huko nyuma pia Baraza la Ushirikiano wa Ghuba ya Uajemi limekuwa likidai
kuwa visiwa hivyo vitatu ni milki ya Umoja wa Falme za Kiarabu, nchi
ambayo iliundwa mwaka 1971 wakati visiwa hivyo vilikuwa katika milki ya
Iran hata kabla ya kuundwa nchi hiyo.
Mawaziri wa Mambo ya Nje wa GCC ambao walilazimika kukutana
Jiddah kwa sababu ya kujadili tishio la ugaidi na kutatua tofauti zao
za ndani, walighafilika na asili ya mjadala na kucheza tena karata butu.
Uzoefu wa miaka 33 ya tangu kuundwa Baraza la Ushirikiano
wa Ghuba ya Uajemi umeonesha kuwa, baraza hilo linaundwa na nchi zisizo
na uwiano na zenye mitazamo tofauti ambazo hazikuweza kutibu majeraha ya
miaka mingi; kwa msingi huo zinatumia uchochezi kwa ajili ya kuficha
udhaifu wao.
GCC linaingilia mambo ya ndani ya Iran kwa kukariri madai
ya umiliki wa visiwa vitatu vya Iran wakati ushahidi na nyaraka za
kimataifa zilizothibitishwa na Umoja wa Mataifa zinaonesha kwamba,
visiwa hivyo ni milki ya Iran.
Mshauri wa Chuo Kikuu cha Umoja wa Mataifa Pirouz
Mujtahizadeh anasema: Nyaraka saba zimetiwa saini kuhusu visiwa vitatu
vya Iran na hata serikali ya Imarati ambayo ni miongoni mwa nchi
wanachama wa baraza la GCC imetia saini nyaraka hizo.
Kwa kuzingatia nyaraka na hati hizo madhubuti inadhihiri
kwamba, kwa kukaririwa madai hayo kuhusu visiwa vitatu vya Tombu Kubwa,
Tombu Ndogo na Abu Mussa katika vikao mbalimbali, GCC imeazimia
kuingilia mambo ya ndani ya Iran kwa kutumia madai yasiyo sahihi kuhusu
visiwa hivyo vya Iran na kupuuza ujirani mwema.
Kung’ang’ana na msimamo huo wa kupotosha historia na
kutegemea nyaraka zisizo sahihi hakuwezi kulifikisha baraza la GCC
kwenye malengo yake.
Kuheshimiana na ujirani mwema ndiyo mambo
yanayopaswa kuwa msingi wa ushirikiano kati ya nchi za eneo hili la
Ghuba ya Uajemi na ushirikiano huo unaweza kuwa msingi wa kumaliza
ukosefu wa maelewano likiwemo suala la visiwa hivyo vitatu.
Kwa upande wao viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran
wamekuwa wakisisitiza mara kwa mara kwamba, siasa za Tehran kuhusu
majirani zake hususan nchi za kando ya Ghuba ya Uajemi, zimejengeka juu
ya ujirani mwema, kuheshimiana na kujiepusha na hatua yoyote ya
kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine.