Na Baraka Mbolembole, Dar es Salaam
Hivi karibuni Rais wa Shirikisho la soka barani ulaya, Michael Plattin amenukuliwa na vichwa vya habari vya magazeti mengi akisema kwamba anataka kuweka sheria ambayo itamaanisha wachezaji 18 katika mechi yoyote itakayochezwa wanatakiwa kuwa Wazawa!
kamati ya ulaya tayari imeshazuia harakati za kufanya wachezaji wa kigeni katika timu kuwa watano, lakini Platin ana uhakika UEFA na EC watafanya kitu kilicho sahihi zaidi kwa manufaa ya soka la barani Ulaya.
Platin ni mchezeja mshindi wakati wa uchezaji wake akiwa na timu ya Taifa ya Ufaransa. Wakati nchi zilizoendelea zikipambana kuhakikisha wachezaji wazawa wanapata nafasi zaidi katika klabu za ndani, nchini Tanzania hali si hivyo.
Klabu zimekuwa na nguvu kubwa kuliko kamati ambazo zinatakiwa kusimamia na kulinda utambulisho wa klabu za ndani. Klabu zimekuwa zikifanya makosa ya makusudi na pengine kulazimisha baadhi ya kanuni kutorekebishwa kwa maslahi yao.
Miaka minne iliyopita, klabu za Tanzania zilikuwa na ruhusa ya kusajili wachezaji wa kigeni kumi ( 10 ) kabla ya kupunguzwa kufikia wachezaji watano. Liko wapi Azimio la Bagamoyo? Mpango maalumu ambao uliundwa miaka mitano iliyopitwa kwa lengo la kuhakikisha wachezaji wa kigeni wanapungua na kufikia watatu.
Kwa misimu mitatu sasa idadi ya wachezaji wa kigeni katika soka la Tanzania imekuwa watano. Kutoka wachezaji 10 hadi watano ilikuwa sawa, lakini idadi hiyo inatakiwa kupunguzwa zaidi na kufikia wachezaji watatu wa kigeni.
Katika michezo ya ufunguzi wa ligi kuu mwishoni mwa wiki iliyopita, Yanga ilitumia wachezaji wanne wa kigeni, lakini wakajikuta wakipoteza mchezo wao dhidi ya Mtibwa Sugar ambao wamesajili wachezaji 28 wazawa. Unapata kitu gani? Achana na mambo ya ubovu wa uwanja wa Jamhuri na rudi katika ukweli wa mambo utagundua kuwa, wachezaji wazawa wanapopata nafasi wanaweza kufanya vizuri.
Simba na Coastal Union zilichezesha jumla ya wachezaji nane wa kigeni wakati zipokutana, walau wao waliweza kuona faida ya kuwa na wageni hao, lakini ni wengi.

Kipre Tchetche, Kipre Bolou na Didier Kavumbagu wote hao walianza katika kikosi cha kwanza cha mabingwa watetezi wa ligi kuu Bara, Azam FC. Ukichunguza utaona Yanga, Simba, Coastal na Azam zilitumia jumla ya wachezaji 15 katika siku ya kwanza ya michezo ya ligi kuu.
TFF imeshindwa kupanga namna ya kuwapatia nafasi wachezaji wazawa kwa kushindwa kuwa na mipango mizuri ya kutengeneza mfumo wa mashindano ambao utawaruhusu wazawa hao kucheza bila presha ya wageni.
Kulikuwa na jaribio kubwa ambalo lilifanywa na baadhi ya timu kwa kutaka idadi ya wachezaji wa kigeni isipungue kutoka watano na kuwa watatu kama ilivyotakiwa kuwa. Klabu hizo ambazo zina watu wengi katika kamati za TFF, huku pia zikiwa na nguvu katika Bodi ya Ligi zilitaka kuona wachezaji zaidi wa kigeni wakiruhusiwa nchini.
Hivyo walitaka idadi hiyo ifikie saba, huku utetezi wao mkubwa ukiwa ni kufanya vizuri katika michuano ya Afrika upande wa klabu.
Kamati, Kanuni, na Sheria za TFF zimekuwa hazina uhakika na wakati mwingine zimekuwa zikizidiwa kwa nguvu za hoja na klabu. Rais wa TFF, Jamal Malinzi tangu ameingia madarakani mwanzoni mwa mwaka huu amekuwa ‘ bize’ kutangaza kuhusu mkatati wa soka la vijana kama njia sahihi ya kukuza na kuinua mpira wa Tanzania.

Rais wa TFF, Jamal Malinzi
Malinzi amekuwa akienda huku na kule mahali ambapo kuna ‘ mwamko wa soka la vijana’ na kutumia mwanya huo kuonyesha kuwa Tanzania inaweza kufanikiwa kufikia mwaka 2019.
Hajawa tayari kufikiria ni namna gani vijana hao wataendelezwa katika misingi ya kimashindano. Iko wapi ligi kuu ya vijana? Iko wapi ligi daraja la kwanza ya vijana. Nafikiri klabu zote zimeagizwa kuwa na timu za vijana na zimefanya hivyo, lakini hao vijana watashindania wapi.
Mizunguko ya Malinzi katika uhamasishaji wa soka la vijana uende sambamba na mawazo chanya ya kutafuta wadhamini ambao watasaidia kudhamini ligi kuu ya vijana na zile za madaraja ya chini.
Tanzania ina vipaji kila mahali na wazazi wamehamasika kuona watoto wao wakijihusisha na soka tofauti na miaka ya nyuma. Unakumbuka vita na Said Sued na mlezi wake Mzee Sued?
Said alikuwa mchezaji kijana zaidi katika ligi kuu ya Tanzania Bara mwaka 2001 akiwa na miaka 17. Simba ilimsajili akiwa kidato cha pili hivyo kufanya mlezi wa mchezaji huyo kumfuata mara kwa mara Said katika mazoezi ya Simba kwa madai kuwa anatakiwa kuwepo shuleni. Hali ni shwari hivi sasa.

Aishi Manula alihamishwa shule kutoka Kilosa Morogoro na kuja Dar es Salaam na klabu ya Azam FC. Upande mwingine klabu zimekuwa na uitikiaji mzuri kuhusu soka la vijana japo si zote, ila TFF imekosa namna ya kuzisaidia klabu hizo kuwaendeleza vijana hao.
Wazo la Copa Coca Cola ni zuri kwa saabu Thomas Ulimwengu ametoka katika mfumo huo lakini angekuwa amepotelea mbali kama asingekuwa na jitihada za kuhakikisha anacheza soka nje ya Tanzania. Malinzi ameanza kuchoka?
Kama atashindwa kulinda utambulisha wa timu za nyumban ambazo katika siku za sasa unaonekana kupotea. Malinzi hataweza kufanikiwa katika chochote.
Nasikia anachunguza hujuma ambazo Taifa Stars inasadikiwa kufanyiwa wakati wa kuwania nafasi ya kufuzu kwa AFCON, 2015, huko ni kupoteza muda kwa kuwa hatajui chochote zaidi ya kile kilicho upande wake wa kushoto.

Kuna hujuma kubwa katika ligi ya ndani labda Malinzi anatakiwa kumaliza matatizo ya ndani ya TFF kwanza kabla ya kudili na Stars kwa sababu kiwango kilichooneshwa na timu kilikuwa ni cha chini.
Simba, Yanga, Azam FC zimekuwa zikiwekeza pesa nyingi kwa wachezaji wa kigeni. Tatizo la wachezaji wa kigeni katika ligi kuu ya Afrika Kusini, PLS limekwisha baada ya SAFA kuweka sheria ambayo huziruhusu klabu kusaini wachezaji wasiozidi watatu wa kigeni. Kitu ambacho kimekuwa kikifanyika kwetu ndicho kinachopoteza nafasi ya Tanzania katika michuano ya Afrika.
Kuwatumia mastaa wachache wa kigeni na kuwaendeleza vijana wenye vipaji wanaochipukia itasaidia kuipatia mafanikio Stars katika siku za usoni.
Hata kama klabu zitasita kukubali hilo kwa sababu ya kushindwa kuwa washindani katika michuano ya kimataifa. Katika utendaji, sheria ni zile ambazo zinawezekana, lakini TFF imeshindwa kuzitumia sheria hizo kwa sababu ya maslahi ya baadhi ya klabu na si mpira wa nchi kiujumla.
Platin anaitetea Ulaya yake, Malinzi anafikiria nini?. Stars itahujumiwa na nani? Labda kiwango chetu cha chini cha kulinda na kuendeleza vipaji vya vijana katika misingi ya ushindani. Lini Stars itakuwa na vijana mazao ya Simba, Yanga, Azam FC na kufanya vyema Afrika?. Tatizo ni nafasi ya Mkurugenzi wa Ufundi.