
Kenneth Roth, Mkurugenzi Mtendaji wa Human Rights Watch amesema hali ya haki za binadamu nchini Misri inatia wasiwasi na kwamba mwezi uliopita na baada ya miaka 25 yeye binafsi alizuiliwa kwa mara ya kwanza kuingia nchini humo.
Roth amebainisha kuwa, kwa sababu kadhaa ikiwemo ya kutumia mfereji wa Suez unaodhibitiwa na Misri nchi nyingi duniani haziikosoi nchi hiyo kutokana na hali mbaya ya haki za binadamu inayotawala nchini humo.kijuzi.blogspot.com
Ameongeza kuwa uhusiano mzuri ilionao Misri na nchi nyingi unazifanya nchi hizo zisiikosoe serikali ya Cairo kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa ukiukaji wa haki za wananchi wa Misri.
Miongoni mwa shutuma kubwa za ukiukaji wa haki za binadamu zinazouandama utawala wa rais wa sasa wa nchi hiyo Abdul Fattah el Sisi ni mauaji ya mwezi Agosti mwaka jana ya zaidi ya raia 800 waliokuwa wamekusanyika katika medani za Rabiatul Adawiyyah na An Nahdhah mjini Cairo na kuwekwa kizuizini maelfu ya waungaji mkono wa Muhammad Morsi, rais wa nchi hiyo aliyeondolewa madarakani na jeshi.
Wakati huo huo kesi ya ujasusi inayomkabili Morsi na viongozi wengine 35 wa harakati ya Ikhwanul Muslimin imeanza kusikilizwa leo katika Mahakama ya Chuo cha Polisi mjini Cairo.
Muhammad Morsi pamoja na viongozi wenzake wa Ikhwanul Muslimin wanatuhumiwa kujasisi dhidi ya Misri kwa maslahi ya madola ya kigeni, kutoa nyaraka za usalama wa taifa na kushirikiana na makundi ya kitakfiri ya ndani na nje ya Misri kwa lengo la kufanya mashambulio ya kigaidi ndani ya ardhi ya nchi hiyo