UN YAKIRI KUWEPO KWA UHUSIANO USHIRIANO WA MAGAIDI SYRIA NA ISRAEL

UN yakiri kuweko uhusiano kati ya magaidi wa Syria na Israel

Umoja wa Mataifa umethibitisha kuweko uhusiano wa karibu na wa moja kwa moja kati ya makundi ya kigaidi nchini Syria na utawala haramu wa Israel.
kijuzi.blogspot.com

 Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na walinda amani wa Umoja wa Mataifa katika miinuko ya Golan ni kwamba, utawala wa Kizayuni wa Israel umekuwa ukitoa misaada ya kijeshi na kilojistiki kwa makundi ya kigaidi yanayopigana na serikali ya Rais Bashar Asad huko Syria. 

Sehemu moja ya ripoti hiyo inasema kuwa, katika wiki za hivi karibuni, wapiganaji wa makundi ya kigaidi waliojeruhiwa vitani wamekuwa wakiingia Israel kupitia miinuko ya Golan kwa ajili ya kupata matibabu.

 Pia ripoti hiyo ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa imefichua kuwa, kundi la kigaidi la Jab'hat an-Nusra mbali na kushambulia makao ya kikosi cha UN huko Golan na kuteka magari, vifaa na askari wa kikosi hicho, pia lilitumia suhula hizo yakiwemo mavazi ya wanajeshi wa UN kwenye vita dhidi ya serikali ya Syria.

 Haya yanafanyika katika hali ambayo, viongozi waandamizi wa makundi ya kigaidi ya Daesh na an-Nusra waliokamatwa katika nchi za Syria na Iraq wamekiri kwamba wamekuwa wakipokea misaada mbalimbali kutoka kwa utawala ghasibu wa Israel.

Kutolewa ripoti hiyo kumethibitisha matamshi ya mara kwa mara ya viongozi wa Syria kwamba Israel imekuwa ikiyafadhili makundi ya kigaidi yanayopigana na serikali ya Damascus.

 Ushahidi zaidi kuhusu ushirikiano wa Wazayuni na makundi ya kigaidi ya Syria umedhihirika zaidi kufuatia ziara ya Kamal Al-Labwani, kiongozi mwandamizi wa kundi linalojiita eti 'Jeshi Huru la Syria' huko Israel siku tatu zilizopita.

 Pia kiongozi mwengine wa ngazi za juu wa magaidi wa Syria Mohamed Badi siku chache zilizopita ametoa taarifa ya kumshukuru Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel, Benjamin Netanyahu, kutokana na kukubali majeruhi wa makundi ya kigaidi kutibiwa katika hospitali za Israel.

Wachambuzi wengi wa eneo hili la Mashariki ya Kati wanakubaliana kwamba, kupata nguvu makundi ya kigaidi na kitakfiri kama vile Daesh, Jab'hat an-Nusra na Ansaru Sharia katika nchi za Iraq na Syria kumetokana na misaada ya kifedha, kijeshi na kiintelijensia yanayopata kutoka nje ikiwemo ile inayotoka Israel, baadhi ya nchi za Kiarabu na zile za Magharibi.

Wajuzi wa mambo pia wanaitakidi kwamba, utawala haramu wa Israel ambao kwa zaidi ya miongo 6 umekuwa ukipora na kuzikalia kwa mabavu ardhi za Palestina, kwa uungaji mkono wa Marekani umeamua kuungana na makundi ya kigaidi Mashariki ya Kati ili kuzusha migogoro na hali ya ukosefu wa usalama ili ulimwengu ushughulishwe na matukio kama hayo na kusahau jinai za utawala huo dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina.

Ni kutokana na ukweli huo, ndio maana wapembuzi wengi wakahoji nia na dhamira halisi ya Marekani ya kupigia chapuo suala la kuundwa muungano wa kimataifa wa kupambana na ugaidi ilihali Washington, Wazayuni na waitifaki wao ndio waasisi na wafadhili wakubwa wa ugaidi sio tu Mashariki ya Kati lakini pia katika maeneo mengi kote duniani.

chanzo;Idhaa ya kiswahili ya Redio Tehrain