Mpango wa utawala wa Kizayuni wa Israel wa kupora hekta mia nne za ardhi za Palestina katika Ukingo wa Magharibi umekabiliwa na upinzani mkubwa katika uga wa kieneo na kimataifa.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban K-moon ameeleza
wasiwasi wake kuhusu suala hilo na kusema kuwa ni utangulizi wa ujenzi
wa vitongoji vipya vya walowezi wa Kizayuni.
Ban amesema ujenzi wa
vitongoji vya walowezi katika ardhi ya Ukingo wa Magharibi huko
Palestina ni kinyume cha sheria za kimataifa na ameutaka utawala wa
Kizayuni kutilia maanani matakwa ya jamii ya kimataifa na kuheshimu
majukumu yake ya kimataifa.
Baadhi ya nchi za Magharibi pia zimechukua msimamo kama huo
wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na kuitaka Israel isitishe mpango wa
kutwaa ardhi zaidi za Palestina.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza
ameeleza kusikitishwa na mpango wa Israel wa kutaka kupora hekta 400 za
ardhi za kusini mwa ardhi za kusini mwa Bait Laham katika Ukingo wa
Magharibi wa Mto Jordan na kusema hatua hiyo inakiuka sheria.
Philip
Hammond amesema ujenzi wa vitongoji vipya unakiuka sheria za kimataifa
na ni kikwazo kikubwa katika njia ya mazungumzo ya kufikia mapatano
baina ya Israel na Wapalestina
. Hammond amesema Uingereza inaitaka
Israel itupilie mbali uamuzi wake wa kutwaa ardhi za Palestina katika
eneo la Bait Laham.
Utawala wa Kizayuni wa Israel umekuwa ukipora ardhi za
Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi kwa zaidi ya miongo sita sasa na
kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika maeneo hayo.
Uporaji
wa ardhi za Wapalestina na kuwalazimisha kuhama makazi yao ni miongoni
mwa siasa zinazotumiwa na utawala ghasibu wa Israel kwa ajili ya
kubadili muundo wa kijamii wa maeneo ya Wapalestina na kujenga vitongoji
vya walowezi.
Siasa hizo daima zinapingwa na makundi ya mapambano ya
ukombozi ya Palestina.
Kuhusu hatua ya sasa ya utawala wa Kizayuni ya kupora hekta
400 za ardhi za Ukingo wa Magharibi, harakati ya Hizbullah ya Lebanon
imetoa taarifa ikisema kuwa, njama hiyo inafanyika kwa shabaha ya
kukamilisha mpango wa kuiyahudisha Palestina.
Taarifa ya Hizbullah
imesema: Wakulima wa Kipalestina, baba na mababu zao wamekuwa wakitumia
ardhi hizo kwa miaka mingi kwa ajili ya kilimo cha zaituni lakini sasa
utawala ghasibu wa Israel umeghusubu maeneo hayo na kuyaunganisha na
ardhi nyingine zinazokaliwa kwa mabavu kwa shabaha ya kutekeza njama
zake za kubadili muundo wa jamii ya Ukingo wa Magharibi.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri pia imelaani hatua hiyo ya
Israel na kusema, kutwaa ardhi hizo za Palestina kunakiuka makubaliano
ya kimataifa na maamuzi ya Kamati ya Pande Nne ya Kimataifa.
Taarifa ya
Wizara hiyo imesema uamuzi huo ni hatua hasi katika mchakato wa eti
amani ya Mashariki ya Kati na kwamba suala hilo linaweza kuwa na
taathira mbaya.
Baadhi ya wataalamu wa mambo wanasema Israel imechukua
hatua hiyo ya kughusubu hekta 400 za ardhi za Palestina kwa shabaha ya
kuficha kushindwa kwake huko Ghaza baada ya kufikiwa makubaliano ya
kusitisha vita na harakati ya Hamas.
Hata hivyo harakati za mapambano za
Palestina zinasema kuwa jibu la uvamizi huo mpya wa Israel ni kudumisha
mapambano dhidi ya maghasibu Wazayuni.
Chanzo;Idhaa ya Kiswahili ya Radio Iran
