WAISLAMU WAITAKA SERIKALI UINGEREZA KUTOLIITA KUNDI LA KIGAIDI "DAESH" DOLA LA KIISLAMU

Cameron atakiwa asiwaite Daesh ‘Dola la Kiislamu’

Waislamu wa Uingereza wameitaka serikali na vyombo vya habari vya nchi hiyo viache kuliita kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh ‘Dola la Kiislamu.


 Kwa mujibu wa gazeti la Guardian linalochapishwa nchini Uingereza kundi la maimamu wa misikiti na wawakilishi wa vituo vya Kiislamu nchini humo wameitaka serikali na vyombo vya habari viache kutumia istilahi ya ‘Dola la Kiislamu’ kulielezea kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIL). 

Katika barua maalumu ya malalamiko iliyosainiwa na shakhsia hao imeelezwa kuwa mwenendo wa kundi la Daesh sio tu hauna uhusiano wowote na mafundisho ya Uislamu bali unakwenda kinyume na mafundisho ya dini hiyo ya Mwenyezi Mungu na kwamba serikali na vyombo vya habari vya Uingereza huwa vinachafua sura ya dini ya Uislamu kwa kuliita kundi hilo ‘Dola la Kiislamu’.

 Barua hiyo imebainisha kuwa kuna watu nchini Uingereza wanaowaghilibu vijana wajiunge na kundi la Daesh na hivyo imeitaka serikali ichukue hatua za lazima kuzuia suala hilo.

 Watiaji saini wa barua hiyo ya malalamiko wamesisitiza kwamba kuanzia sasa watakuwa wanaliita kundi la Daesh ‘Dola lisilo la Kiislamu’ (Unislamic State). 

Mara kadhaa na hasa katika kikao cha mwezi huu cha bunge la Uingereza, Waziri Mkuu wa nchi hiyo David Cameron na viongozi wengine kadhaa waandamizi wa serikali yake wamekuwa wakiliita kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh ‘Dola la Kiislamu’…/