
Na Baraka Mbolembole, Dar es Salaam,
Kitu kizuri huleta furaha ya siku zote katika dunia, uzuri wake huwa wa kuendelea hata kama kitu cha zamani. Thamani ya kitu kizuri ni ‘ shida’ kukishusha chini kutokana na ubora wake. Kitu kikiwa kizuri ni ‘ pambo’ katika dunia hii. Yanga wameendeleza ‘ utawala’ katika Ngao ya Jamii baada ya ushindi wa kuvutia wa mabao 3-0 dhidi ya mabingwa wa Bara, Azam FC katika mchezo uluipigwa uwanja wa Taifa, Jumapili hii. Yanga ndiyo Wafalme tena wa Ngao ya Jamii, hawana mwisho kushinda.
Geilsons Santos ‘ Jaja’ alifunga mara mbili mara baada ya kuanza kwa kipindi cha pili na kuzima ‘ wasiwasi’ wote ambao ulitanda juu yake kama kweli ni mshambulizi-mfungaji. Amedhihirisha kuwa yeye ni Mbrazil mchezaji ambaye nilimuamini tangu Maximo alipoamua kumfanya ‘ kiongozi wa safu ya mashambulizi’ katika mfumo wa 4-5-1.
Timu ambayo ilionekana bora na ngumu kupitika katika kipindi cha kwanza ilikuwa ‘ nyanya’ nusu ya pili ya mchezo. Azam waliibana Yanga licha ya kushambuliwa mara nne katika kipindi cha kwanza, ilionekana kama vile Marcio Maximo amechemsha katika mfumo wake baada ya kushuhudia timu yake ikishindwa kutengeneza nafasi. Jaja alionekana kutengwa huku mshambulizi namba mbili ambaye alitakiwa kucheza nyuma kidogo ya Jaja akishindwa kutimiza majukumu yake ipasavyo.
Maximo ameshinda taji lake la kwanza akiwa kocha, na hilo limekuja baada ya kutua Yanga. Alimuanzisha kiungo wa timu ya Taifa ya Tanzania, Said Juma baada ya kukosa huduma ya kiungo wake Mbrazil, Andrey Coutinho. Yanga walimiliki mpira na kiungo mchezesha timu Haruna Niyonzima alikuwa na kasi, nguvu na ufundi ambao uliifanya safu ya kiungo ya Yanga kucheza mchezo wa kasi. Nizar Khalfan alianza katika kikosi cha kwanza, Azam ilionekana kutawala mchezo licha ya kutotengeneza nafasi za kufunga.
Maximo alimtoa Juma na kumuingiza Hassan Dilunga katika dakika ya 38. Mabadiliko hayo yalilenga kuimarisha eneo la katikati ya uwanja ambalo lilionekana kuzidiwa baada ya Nizar kuanza kuchoka. Mrisho Ngassa alikuwa katika kiwango cha juu licha ya upinzani mkali kutoka kwa Erasto Nyoni. Ngassa alikaribia kufunga bao la ufundi kwa mpira wa umbali mrefu kutoka winga ya kulia, lakini golikipa Mwadini Ally aliuona ujanja wa winga huyo wa Taifa Stars.
Jaribio la kwanza la Jaja ilikuwa ni kupiga ‘ kishuti mtoto’ ambacho kiliokotwa na Mwadini mwishoni mwa kipindi cha kwanza, lakini ilikuwa ni onyo ambalo halikufanyiwa kazi na walinzi wa Azam kwani ‘ walitorokwa’ pasipo kukijua. Kama angepiga mpira ule kwa nguvu angefunga, si rahisi kumuona akipiga mpira nje. Yanga walikuwa makini kila idara, safu ya ulinzi chini ya golikipa, Deogratius Munishi ilijiamini huku umakini ukiwa mkubwa katika uchezaji wao. Juma Abdul alimbana, Lieonel Saint kila alipojaribu kuisaidia timu yake, Oscar Joshua alikuwa mgumu kwa Kipre Tchecthe, wakati Nadir Haroub na Kelvin Yondan walihakikisha hakuna nafasi ya wazi ambayo Kavumbagu anaipata.
Mara moja Kavumbagu alioneka kuwa tishio wakati alipotaka kuwahi pasi ya kupenyeza ya Salum Abubakary lakini alibanwa kifundi na Nadir ambaye alicheza ‘ tackling’ nzuri ndani ya eneo la hatari akiwa mchezaji wa mwisho. Kipre alitolewa baadae kipindi cha pili, na hivyo pia ilikuwa kwa Saint.
Kuingia kwa Saimon Msuva mara baada ya kuanza kwa kipindi cha pili kuliimaliza kabisa Azam katika eneo la kiungo. Dilunga alikuwa akikimbia na mipira upande wa kulia na kumpa wakati mgumu Shomari Kapombe ambaye hakupanda hata mara moja. Akiwa amechukua nafasi ya Nizar, Msuva alicheza kama kiungo wa kushoto, majukumu mapya ambayo aliyatimiza vizuri . Alikimbia na mpira katika winga ya kushoto na kupiga pasi ya kupenyeza kwa ‘ mchezaji bora wa mechi kwa upande wangu’ Niyonzima ambaye alipiga krosi kwa mguu wa kushoto iliyomaliziwa na Jaja katika dakika ya 53.
Ngassa ambaye alicheza kama msaidizi wa karibu wa Jaja katika kipindi cha pili alimpatia pasi muruha Jaja ambaye alipiga mpira wa juu kiufundi akimuacha kipa Mwadini akiutazama bila kujua cha kufanya. Bao hilo la pili katika dakika ya 65 liliimaliza kabisa Azam. Kocha, Joseph Omog akaamua kufanya mabadiliko yake ya kwanza kwa kuwaingiza uwanja Hamis Mcha na Kelvin Friday lakini tayari alikuwa amechelewa. Kikosi chake kilisambaratishwa na bao hilo na Niyonzima akawa anapiga pasi zinazofika huku akiichezesha timu yake.
Hussein Javu ambaye aliingia kuchukua nafasi ya Jaja, alipiga pasi ndefu kwa Msuva ambaye alifunga moja ya mabao mazuri zikiwa zimesalia dakika tatu mchezo kumalizika. Yanga wameendeleza ‘ utamaduni wa kuishinda Azam kila katika mchezo wa vikombe’ waliifungwa mabao 2-0 katika fainali ya Kagame Cup, 2012 na waliichapa bao 1-0 katika mchezo wa Ngao ya Jamii mwaka uliopita. Azam ilizidiwa kutokana na kasi ya Yanga katikati ya uwanja. Jaja ataendelea kuwafunga , apewe heshima yake. Watu hitoa sifa nyingi nzuri kwa kilicho bora, kitu kizuri hakitoki nje kujitembeza.