BUNGE Maalumu la Katiba limepata mtikisiko kutokana na baadhi ya wajumbe kumshutumu Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud ambaye alipiga kura ya hapana kinyume cha matarajio yao na hivyo kutolewa chini ya ulinzi mkali wa askari wa Bunge.
Hilo lilitokea baada ya Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta kuita jina la mwanasheria mkuu huyo kwa ajili ya kupiga kura ya wazi kwa vile hakuwepo bungeni wakati upigaji kura huo ulipoanza siku mbili zilizopita.
Kinyume cha matarajio ya wajumbe wengi wakiwamo kutoka visiwani Zanzibar, Masoud alipiga kura yake akipinga baadhi ya ibara katika rasimu iliyowasilishwa na Kamati ya Uandishi hivi karibuni.
Hali ilivyokuwa
Kutokana na kura aliyopiga ambayo ilizua hasira kwa wajumbe kutoka visiwani humo, baada ya Sitta kuahirisha kikao cha Bunge, baadhi yao walionekana wakimsogelea, hatua iliyozua hofu kuhusu usalama wake.
Tukio hilo lilidumu kwa dakika kadhaa, ambapo wajumbe hao hawakutoka nje hadi walipohakikisha wanamsubiri atoke kisha wamfuate ingawa baadhi yao walikuwa nje.
Hali hiyo ililazimu askari wa Bunge kuchukua tahadhari na kumuwekea ulinzi mkali na kumtoa nje kupitia lango wanalotumia viongozi wakuu kuingia na kutokea bungeni.
Hata hivyo, dakika zaidi ya 20 mara baada ya Bunge kuahirishwa saa nne asubuhi, hakutoka nje ambako wajumbe hao walikuwa wakimsubiri.
Baada ya muda huo ndipo askari hao walimtoa nje ya Ukumbi wa Bunge ambapo alikuwa amekaa kwenye moja ya vyumba vilivyomo ndani ya ukumbi huo ili kusubiri hali iliyokuwepo nje ya hasira za wajumbe itulie.
Hatimaye alitoka chini ya ulinzi akiwa ameongozana na Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Pandu Ameir Kificho pamoja na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idi.
Askari hao zaidi ya wanne wa kike na wa kiume pamoja na usalama wa taifa, walihakikisha anapanda gari kwa usalama bila kuguswa. Gari alilopanda lenye namba za usajili ZNZ 6197 linatumiwa na Kificho.
Alitokea geti analotumia Waziri Mkuu kuelekea nje ya Bunge bila kufahamika wapi alikoelekea ingawa wajumbe hao walionekana wakikaa makundi makundi kujadili kilichotokea.
Mwanasheria Mkuu
Wakati akipiga kura, mwanasheria huyo alisema anapinga ibara ya pili, ambayo inahusu eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ya tisa inayosema Katiba ni Sheria Kuu katika Jamhuri ya Muungano kwa mujibu wa masharti yaliyowekwa na Katiba.
Pia, mjumbe huyo aliikataa ibara ya 86 inayohusu uchaguzi wa rais iliyopo katika sura ya nane katika rasimu, huku akitaja sura ya saba na ibara ya 70 hadi 75 zinazohusu muundo wa Jamhuri ya Muungano ambazo msingi mkuu wa ibara hizo ni muundo wa Serikali mbili.
Alizitaja pia, ibara za 128 na 129 zilizoko katika sura ya 10 ya rasimu pendekezo huku zikieleza muundo wa madaraka ya Bunge la Jamhuri ya Muungano.
Pia, alisema anapinga sura ya 11 pamoja na kuzikataa ibara ya 158, 159, 160 na ya 161 ambayo inazungumzia Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Baraza la Mapinduzi la Zanzibar na Baraza la Wawakilishi.
Kwa upande wa sura ya 10, Masoud alizikataa ibara zinazoanzia 142 hadi 151 ambazo kimsingi zinahusu uongozi wa Bunge la Muungano, ambapo aliikataa ibara iliyoongezwa katika ibara ya 70.
Hatua ya Masoud kupiga kura ni kutokana na unyeti wa hatua hiyo ya kuamua hatma ya rasimu pamoja na kutoshiriki tangu mwanzo ililazimu apige kura ili kuweka uhalali wa pande mbili za Muungano kushiriki.
Hata hivyo, pamoja na hatua ya wajumbe hao kuzomea, Sitta alituliza upepo na kuwataka kumuacha kwani amepiga kura kama mjumbe na si kwa ajili ya nafasi yake.
Wajumbe wakasirika
Kutokana hatua yake ya kupinga rasimu ambayo ilisababisha kura za hapana kuongezeka, baadhi ya wajumbe walitoa taarifa kwa mwenyekiti kuonesha hisia zao kutokana na hali hiyo.
Miongoni mwao ni, Yahaya Kassim ambaye pia, ni Mbunge wa Chwaka kupitia CCM, alisema anashangazwa na uamuzi wa mwanasheria mkuu huyo akisema hakushiriki katika kujadili rasimu, lakini amekuja na kuipinga.
Alisema mwanasheria huyo ameonesha usaliti kwa kupingana na Serikali yake kutokana na hatua yake ya kupiga kura ya kuikataa rasimu hiyo.
Mjumbe huyo alionesha hisia zake kuhusu suala hilo na kwenda mbali zaidi kwa kueleza kwamba mwanasheria mkuu hakua mgonjwa, bali aliamua tu kutoshiriki katika mchakato huo kwa sababu ya jeuri yake kuonesha kuwa ni msomi.
Alimwita kuwa ni mtoro ambaye walitegemea awepo tangu mwanzo wa Bunge, lakini hakufanya hivyo huku akihoji ana maslahi gani kwa Wazanzibari.
Pia, Hamad Rashid Mohammed alisema kuwa kwa vile ameamua kufanya hivyo, kama Rais Dk. Ali Mohamed Shein aliyemteua ataamua kumfukuza ni sawa.
Hamad ambaye pia ni Mbunge wa Wawi kupitia CUF, alisema mtu hakatazwi kutoa maoni yake, lakini kwa mtu kama mwanasheria mkuu si sahihi.
"Tulitegemea kuwa yeye kwa vile ni mwakilishi wa Serikali, angepata ushauri au angewaomba ushauri kutoka kwa wajumbe, lakini badala yake ametoa kile alichodhamiria.
"Kwa kweli ameturudisha nyuma wakati mambo mengi tumeshafanya, na kufanya hivyo itabidi Rais apime kama kumuondoa sawa hiyo si kazi yetu kumuondoa, ila naona kwa hatua aliyochukua hatufai kabisa," alihamaki Hamad.
Itakumbukwa kuwa Masoud ambaye pia ni mjumbe kwenye Kamati ya Uandishi inayoongozwa na Mwenyekiti, Andrew Chenge alidaiwa kujitoa katika mchakato huo.
Jana ilikuwa siku ya tatu kwa wajumbe ambao hawakuwepo siku mbili zilizopita za kupigia kura rasimu hiyo, huku matokeo yakitarajiwa kutolewa wakati wowote.