
Rais JAKAYA KIKWETE amesema kuwa TANZANIA imekubali kuwa msuluhishi wa mgogoro wa kisiasa ndani ya chama tawala cha SUDAN Kusini cha Sudanese People’s Liberation Movement -SPLM, mgogoro ambao umesababisha kuzuka kwa vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.
Hata hivyo, Rais KIKWETE amesema kuwa usuluhishi huo utakuwa wa kichama ambapo Chama cha Mapinduzi -CCM ndicho kitaongoza usuluhishi huo mjini ARUSHA na kuwa jitihada hizo za TANZANIA hazitaingilia mazungumzo ya kusimamisha mapigano nchini humo yanayoendelea huko ADDIS ABABA, ETHIOPIA.
Rais KIKWETE amesema kuwa ulikuwa uongozi wa SPLM na hasa Mwenyekiti wa Chama hicho, Rais SALVA KIIR ambao wameiomba TANZANIA kusaidia jitihada za kisiasa za kupatanisha pande ambazo zinavutana na kutofautiana ndani ya SPLM.
Rais Kikwete ametangaza jitihada hizo wakati alipohutubia wananchi na kupitia kwenye Sherehe ya Kuzima Mwenge wa Uhuru, Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere na Kilele cha Wiki ya Vijana kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini TABORA.