Brazil, chini ya himaya mpya ya Kocha
Dunga, walitawala, walitamba na kuwachakaza Wenyeji wao Turkey kwa Bao
4-0 ndani ya Atatürk Olimpiyat Stadı Jijini İstanbul kwenye Mechi ya
Kimataifa ya Kirafiki iliyochezwa Jumatano Usiku.
Brazil walipata Bao lao la kwanza Dakika ya 20 baada ya pasi ndefu ya
Fernandinho kushushwa kifuani na Neymar na kuambaa nayo ndani ya Boksi
na kuachia shuti lililomshinda Kipa Demirel
Bao la pili la Brazil lilifungwa Dakika ya 24 baada ya krosi ya Fulbeki wa Kulia, Danilo, kuguswa na Beki wa Uturuki Kaya na pengine kumparaza Sentafowadi wa Brazil Luis Adriano na kutinga.
Hata hivyo, Bao hilo liliandikwa kama ni Goli la kujifunga wenyewe Mfungaji akiwa Kaya.
Neymar alifanya kazi kubwa na ufundi mkubwa kwa kuihadaa ngome ya
Uturuki na ngoma kumfikia Willian aliefunga na kuipa Brazil Bao la 3
katika Dakika ya 44.
Hadi Mapumziko Uturuki 0 Brazil 3.
Dakika ya 61, uchawi wa Neymar ulionekana tena baada ya kufunga Bao
safi alipolishwa Winga ya kushoto na kutumbukia ndani ya Boksi na
kuihadaa Difensi nzima ya Uturuki na kufunga Bao la 4 kwa utaalam
mkubwa.
Matokeo haya yanaendeleza uteja wa Uturuki kwa Brazil kwani
wameshakutana mara 6 na Brazil kushinda Mechi 5 na Sare moja ya 0-0
Mwaka 2007.
Pia, himaya mpya ya Kocha Dunga imeendelea kwa wimbi la ushindi wa
Mechi zake zote 5 tangu atwae madaraka mara baada ya kumalizika Fainali
za Kombe la Dunia huko Brazil kwa kuzitandika pia Colombia, Ecuador,
Argentina na Japan huku wakifunga jumla ya Bao 12 bila kufungwa hata
moja na Neymar akipiga Bao 7 kati ya hizo.
Mechi inayofuata kwa Brazil ni hapo Jumanne Novemba 18 huko Vienna watakapocheza na Wenyeji wao Austria.
VIKOSI VILIVYOANZA:
Turkey (Mfumo 4-4-2): Demirel; Kaya, Irtegun, Koybasi, Tufan; Altintop, Topal, Kisa, Turan; Bulut, Erding.
Brazil (Mfumo 4-3-3): Diego Alves; Danilo, Miranda, David Luiz, Filipe Luis; Luiz Gustavo, Fernandinho, Oscar; Willan, Luiz Adriano, Neymar