![]() |
Katibu wa CCM mkoa wa Singida, Mary Chatanda |
Vigogo wawili wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wilayani hapa nusura wazichape hadharani baada ya kutoleana maneno ya kashfa.
Vigogo hao ni Katibu wa CCM mkoa wa Singida, Mary Chatanda ambaye
pia ni Mbunge wa Viti maalumu na Katibu wa CCM Wilaya ya Korogwe,
Mwanaidi Mbisha.
Kufuatia tukio hilo, makada wa chama hicho wilayani Korogwe wamelaani na kusema limewaondolea sifa viongozi hao.
Wametishia kuandamana kama chama hakitachukua hatua dhidi yao
kwani licha ya viongozi hao kujifedhehesha lakini pia wamekidhalilisha
chama.
Mmoja wa makada hao ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini
alidai chanzo cha ugomvi huo ni Chatanda kumtuma kijana mmoja (jina
linahifadhiwa) kumnunulia maziwa kwa kutumia gari la Mbisha bila
kumjulisha mwenyewe.
Alisema baada ya Mbisha kuona gari lake linatoka bila idhini yake,
alitoka nje na kuhoji nani aliyeamua kuchukua gari lake bila ruhusa yake
wakati funguo akiwa nazo yeye.
Ilidaiwa kuwa baada ya Mbisha kuhoji ndipo Chatanda alipodakia na kuanza kumtolea mwenzake maneno ya kashfa.
Kada huyo alisema nyumba ya Chatanda na Mbisha zimekaribiana.
“Ukweli pale yalikuwapo maneno makali sana huyu mama Chatanda
akimtukana mwenzake kumuita masikini, fukara huku akisema anaweza
kumhamisha na maneno mengine si busara kutaja. Wakati huo wote Mbisha
alikuwa akitaka kujua gari lake liliondokaje wakati funguo yake anayo,”
alisema kada huyo.
Inadaiwa kuwa licha ya chanzo cha ugomvi kuwa ni gari lakini jimbo
ndiyo linalogombewa. “Pale kuna siasa tena zile chafu, Chatanda
anatarajia kuwania ubunge sasa anahisi kwamba Mbisha hawezi kumuunga
mkono katika lengo lake hilo hivyo alikuwa akimshughulikia angalau aweze
kusalimu amri, lile la gari lilijitokeza tu,” alisema kada mwingine.
Kufuatia patashika hiyo, Mbisha alilazimika kupiga simu polisi na baada ya kufika walimkuta Chatanda akiendelea kufoka.
Habari kutoka vyanzo vya habari ndani ya polisi zinasema waliutatua
mgongano huo baada ya kuthibitisha kuwa funguo zilizotolewa zinatumika
kufungua gari lingine.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Frasser Kishai, alikiri kutokea kwa tukio hilo.
Mbisha alipohojiwa na gazeti hili alisema Oktoba 30, majira ya saa
2.25 asubuhi akiwa nyumbani kwake alisikia gari lake likiwashwa na
alipomtuma kijana wake kufuatilia, kijana aliyetoka na gari alimjibu
amepewa funguo na katibu wa CCM Korogwe vijijini, Jumanne Kitundu na
hapo ndiyo chanzo cha kutukanwa na Chatanda.
“Yule mama licha ya kunitolea matusi mazito hadharani, lakini
alinitishia kunifukuzisha kazi na kuhoji vipi sijahamishwa wakati
alishafanya mipango ya kuhamishwa katika wilaya hiyo…,” alisema Mbisha.
Naye Chatanda alipoulizwa kwa njia ya simu kuhusu tukio hilo,
alijibu kwa mkato kwamba hana maelezo kwa jambo ambalo halifahamu.
“Mimi sijui chochote, habari za Mbisha, muulize Mbisha mwenyewe…
Mbisha ni Mbisha na mimi ni Chatanda sawa," alisema na kukata simu.
Hata hivyo, katibu wa CCM Mkoa wa Tanga, Shijja Othuman, alipoulizwa alidai kuwa hana taarifa.
CHANZO:
NIPASHEA