
Simba imetangaza kumuhitaji winga huyo ambaye ameonyesha kiwango
cha juu tangu mwaka jana huku akionekana kuwa mkombozi wa Yanga msimu
huu.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, kocha msaidizi wa Yanga
Salvatory Edwarad alisema hawafikirii kumuuza Msuva kwa kuwa ni mmoja wa
wachezaji muhimu kwenye kikosi hicho.
Alisema ana uhakika "wakubwa" wake wa kazi hawatafikiria kumuuza
nyota huyo kwa klabu za ligi kuu na kama itatokea ulazima wa kufanya
hivyo labda kwa ofa kutoka nje ya nchi.
"Hayo ni maneno ya tu ambayo tunayasikia lakini Msuva ni mchezaji
mkubwa na muhimu (hivyo) kamwe Yanga haitafikiria kumuuza kwa kipindi
hiki; tena kwa timu ya ligi kuu," alisema.
Vyombo mbalimbali vya habari vimewanukuu baadhi ya viongozi wa
Simba wakisema watapeleka barua Yanga kwa ajili ya kutaka kumsajili
winga huyo hatari.
Msuva ambaye pia yupo kwenye kikosi cha timu ya taifa 'Taifa Stars', amekuwa akionyesha kiwango kikubwa kwenye kikosi cha Yanga.
Hivi karibuni kocha mkuu Marcio Maximo aliiambia Nipashe kuwa nyota
huyo ni hazina kwa taifa na mmoja wa wachezaji muhimu kwenye kikosi
chake.
Katika mchezo uliopita wa ligi kuu ya Bara dhidi ya Mgambo JKT,
Msuva aliingia kutoka benchini katika kipindi cha pili na kufunga mabao
mawili yaliyoipa timu yake ushindi wa 2-0.
Kwa sasa viongozi wa Yanga wapo makini na karibu na mchezaji hiyo
ili kuhakikisha harubuniwi na timu pinzani, uchunguzi wa Nipashe
umegundua.
CHANZO:
NIPASHE