CHELSEA, ARSENAL MANCITY KUSHUKA DIMBANI LEO

BAADA ya Jumanne kupigwa Mechi 6 za Ligi Kuu England, Jumatano Usiku zitacheza Timu 8 zilizosalia katika Mechi 4 ambazo wapo Vinara Chelsea wakiwa kwao Stamford Bridge kuivaa Tottenham wakati Mabingwa Watetezi Manchester City watakuwa Ugenini kucheza na Sunderland.

Chelsea, chini ya Meneja Jose Mourinho, watacheza na Tottenham bila ya Straika wao Nambari Wani Diego Costa ambae yupo Kifungoni baada ya kuzoa Kadi za Njano 5 na hivyo kulazimika kuikosa Mechi Moja.

Hata hivyo, Chelsea wana rekodi nzuri na Tottenham ambao hawajaishinda Chelsea tangu Aprili 2010.

Mechi nyingine Jumatano Usiku ni huko Emirates ambako Southampton, Timu ambayo iko nafasi ya 3, itawavaa Wenyeji Arsenal ambao wako Nafasi ya 6 Pointi 6 nyuma ya Southampton ambayo pia ilishinda Mechi yao ya mwisho na Arsenal hapo hapo Emirates na kuwabwaga nje ya Capital One Cup.

Nao Mabingwa Man City wako Ugenini huko Stadium of Light kucheza na Sunderland ambao kawada hupata matokeo mazuri dhidi ya City.

Huko Goodison Park, Everton wanaikaribisha Hull City ambayo imerudi nyuma baada ya kuanza Ligi vizuri.