RUNGU LA UEFA LAIKUMBA LIVERPOOL ROMA NA AS MONACO


KLABU 7, zikiwemo Liverpool, AS Monaco na AS Roma, zimo kwenye uchunguzi wa UEFA kwa kukiuka Kanuni za FFP [Financial Fair Play] baada kuzidisha Matumizi kwa ununuzi wa Wachezaji wapya na Mishahara ya Wafanyakazi wao.

Kwa mujibu wa Kanuni za FFP, ambazo Klabu zinazocheza Mashindano ya UEFA hupaswa kuzifuata, kila Klabu inatakiwa kuwa na Matumizi yasiyozidi Mapato yao.

Mapato hayo ni yale tu yanayotokana na Viingilio vya Mechi, Matangazo ya TV na Biashara nyingine na si kupata ruzuku kutoka kwa Wamiliki wao.

Klabu nyingine ambazo zinachunguzwa ni Sporting Lisbon, Inter Milan, Besiktas na Krasnodar.

Kwa mujibu wa UEFA Klabu hizo 7 zilipata Hasara kwenye Mahesabu yao yaliyoishia Miaka ya Fedha ya 2012 na 2013 na zimelazimishwa kupeleka upya Taarifa zao za Mahesabu yanayoishia Februari 2014 ili wafanyiwe tathmini.

Klabu nyingine 6, Sparta Prague, Hull, Lyon, Panathinaikos, Ruch Chorzow na Wolfsburg, ambazo zote zinacheza EUROPA LIGI Msimu huu, zimetakiwa kupeleka Mahesabu yao upya ili kuonyesha wanakaribia kupata Faida.

UEFA ilianzisha FFP Mwaka 2011 ili kudhibiti Klabu kutumia Fedha kupindukia kwenye Uhamisho wa Wachezaji na Mishahara na Adhabu kubwa kwa Klabu zinazokiuka ni kutocheza Mashindano ya UEFA Ulaya, Faini na Klabu kuminywa kusajili Wachezaji wengi.

Mwezi Mei, rungu la kwanza la UEFA kwa ukiukwaji wa FFP lilitua kwa Manchester City na Paris Saint-Germain kwa kupigwa Faini na kubanwa katika Usajili wa Wachezaji wapya