TAZAMA VIDEO....AY ; NIMEKUWA WAKALA WA WASANII




Katika mahojiano na safu hii ambayo huwa inarushwa kupitia Global Tv Online kwenye Kipindi cha Mtu Kati, AY aliweka wazi kuwa anafanya muziki kwa ajili ya watu wote.Mwandishi: Unakumbuka nini kupitia kundi lako la zamani la East Coast Team ambayo sasa hivi haipo tena? 

AY: East Coast Team bado ipo, kitu ambacho nakumbuka sisi tulikuwa marafiki na muziki ulitufanya tukawa kama ndugu, nilitoka mwaka 2006 kwa ajili ya tofauti za kimisimamo na kimtazamo, baadaye MwanaFA naye akaja kutoka.

Baada ya kuachana bado tulikuwa tunawasiliana na kutembeleana lakini kila mtu anafanya kazi katika njia yake na mpaka sasa hivi wenyewe bado wanaendelea kama East Coast Team pia kuna ‘project’ ambayo tutakuja kuifanya pamoja mwakani.

Mwandishi: Inasemekana uko zaidi na MwanaFA kuliko GK kuna nini hapo kati?
AY:  Wakati natoka nilibakia kuwa AY na MwanaFA kama MwanaFA na mimi na MwanaFA ni washikaji kama ‘brothers’, ndiyo maana tumeshirikiana kwenye project nyingi zaidi baada ya kutoka nje. Sisi siyo kundi lakini kila mtu ni mwanamuziki wa kujitegemea.

Mwandishi: Mbali na muziki wewe ni meneja ambaye unamiliki wanamuziki wengi ndani na nje ya Tanzania, kwa sasa una wasanii wangapi?

AY: Sasa hivi nimekuwa wakala, kampuni yangu inafanya kazi ya uwakala na wasanii wengi nje na ndani. Miongoni mwao ambao nimeshawahi kufanya nao kuna Nameless, Stereo, Ommy Dimpoz, Chameleone, P-square na wengine wengi. Kampuni kama hizo zipo katika kila nchi kwa hiyo na mimi nikaona bora nifungue. 

Mwandishi: Changamoto gani unakumbana nazo katika biashara zako?

AY: Biashara yoyote ina changamoto na inakufanya akili yako inakuwa inapanuka zaidi na unaweza kujifunza mbinu nyingi kupitia changamoto uliyoipata. Kiukweli tunajitahidi mimi pamoja na wenzangu tunaona jinsi matunda ya kazi yetu tunayoifanya.

AY akiwa ndani ya studio za Global TV Online na prizenta Pamela Daffa 'Pam D'.

Mwandishi: Unahisi ni sababu gani zinawafanya vijana wengi kushindwa kutoboa kimataifa?

AY: Hii kitu nilikuwa naiangalia tangu zamani ndiyo maana naona nikiendelea kushikilia vitu vya zamani nilivyokuwa navifanya nisingeweza kufikisha vitu ambavyo vinafanyika leo.

Nilivyoingia kwenye muziki nilikuwa nataka siku ambayo naacha muziki watu wanikumbuke kwa kitu fulani, lazima muziki ubadilishe maisha yangu ndiyo maana unaona najitahidi kuwavuta wasanii wenzangu kuwapa chaneli na netiweki zingine kwa ajili ya kwenda mbali zaidi.

Mwandishi: Nini siri ya mafanikio yako?

AY: Vyote hivi ni kuipenda kazi uwe na heshima nayo yaani ujiheshimu na pia uwe na mtandao ujue jinsi ya kufahamiana na watu.

Mwandishi: Ulijisikiaje kufanya kazi na Sean Kingstone?

AY: Nilijisikia vizuri sana kwani mefanya kazi na msanii ambaye zamani nilikuwa namuona kwenye runinga sikuwa na mawazo ya kuja kukutana naye na kufanya naye kazi, kizuri zaidi yeye ndiyo alipendekeza nifanye naye kazi nakumbuka alikuwa amekuja hapa na akaona kazi zangu na alivyokwenda kufanya mahojiano kwenye redio nilikuwa nasikiliza siku hiyo  nikashangaa ananitaja mimi bila kujua.

Mwandishi: Ni hatua gani ambayo unaikumbuka imekupa mafanikio?

AY: Nakumbuka Profesa J wakati anazindua albamu yake ya Machozi, Jasho na Damu, akanipa kolabo katika albamu yake wakati nikiwa na ngoma ya Raha Tu, akaniambia wimbo unaitwa Nawakilisha nataka ‘verse’ kesho yake nikawa tayari basi tukaanza kuzunguka na ndiyo ‘tour’ iliyonifanya nikaanza kufahamika Tanzania nzima, kufahamiana na watu zaidi na mpaka leo tunashirikiana vizuri.

Mwandishi: Sasa hivi umesimama kutoa albamu, unakumbuka una albamu ngapi mpaka sasa?

AY: Nimeacha kutoa albamu tangu mwaka 2006 miaka 8 iliyopita, ya kwanza ilikuwa inaitwa Raha Kamili 2003, Hisia Zangu 2005, Habari Ndiyo Hiyo niliyoifanya na MwanaFA. Nafanya muziki kwa ajili ya watu wote, nafanya kama AY lakini bidii zangu pia hata wasanii  wengine wanafaidika nazo, tusapotiane tuweze kusonga mbele, tuwe na upendo kati yetu, tusipandikiziane chuki kati  ya wasani kwa wasanii ili twende pamoja, tufike mbali zaidi.