BAADA YA vuta nikuvute ya Miaka kadhaa hatimae Klabu ya Liverpool imefanikiwa kuinunua Nyumba ya mwisho iliyokuwa kikwazo katika mipango yao ya kupanua Uwanja wao wa Anfield. Nyumba hiyo itabomolewa kuanzia Jumatatu ili Uwanja wa Anfield upanuliwe na kubeba Watu kutoka 45,500 wa sasa hadi kufikia Washabiki 59,000. Ujenzi huo utakaogharimu Pauni Milioni 100 utaanza kwa Awamu ya Kwanza ya upanuzi wa Jukwaa Kuu ambalo litaongezwa Ghorofa ya Juu ili kuongeza Viti 8,300. Baada ya hapo, Jukwaa la Anfield Road litaongezwa Viti 4,800. Ujenzi huu unatarajiwa kumalizika kabla ya Msimu wa 2016/17 kuanza na pia utahusisha ujenzi wa Kumbi zaidi za Mikutano, Mgahawa na Eneo la kuegesha Magari. Licha ya kuiongezea Mapato Liverpool, pia upanuzi huu utaiwezesha Anfield kukubalika kutumika kwa Mechi za Kimataifa ambazo kwa sasa haziruhusiwi kwa vile upo chini ya Viwango vya UEFA. UEFA hutaka Viwanja vya Mechi za Kimataifa visiwe na chini ya Viti 50,000, viwe na Vyumba vya Kulala Wageni pamoja na kuwa na miundombinu kadhaa yenye viwango stahiki vikiwemo Vyumba vya Kubadili Jezi Timu na Waamuzi.