
Dirisha la usajili barani ulaya limebakiza takribani masaa 48 kabla ya
kufungwa, na kama ilivyo ada tetesi za usajili wa wachezaji tofauti
zimezidi kushika kasi.
Klabu ya Manchester United ambayo imekuwa na udhaifu kwenye kikosi hasa
kwenye maeneo ya kiungo na beki wa kati, leo hii Manchester United
wameshindwa kukanusha taarifa kwamba wametuma ofa ya £37m kwa Borussia
Dortmund na kuanza mazungumzo kwa ajili ya usajili wa beki Mats Hummels. Inaaminika ikiwa usajili huo utafanikiwa basi beki wa Dinamo Kiev Aleksandar Dragovic atanunuliwa kurithi mikoba ya Hummels.
United wamekuwa wakihusishwa na usajili wa Mats Hummels tangu wakati wa
dirisha la kiangazi lakini walikutana na kizingiti cha Dortmund kugoma
kumuuza beki huyo mshindi wa kombe la dunia mwaka 2014, lakini sasa
klabu hiyo ambayo ipo kwenye mkia wa msimamo wa Bundesliga inaonekana
kuwa tayari kumuuza beki huyo ambaye pia alikuwa akihusishwa na kutakiwa
na Arsenal.
Wakati huo huo mchezaji na nahodha msaidizi wa Man United Darren
Fletcher anatarajiwa kujiunga na West Ham United kwa uhamisho wa bure na
anategemewa kusaini mkataba wa miaka miwili na nusu ikiwa kila kitu
kitaenda kama kilivyopangwa.