
Waziri wa Mali Asili na Utalii, Lazaro Nyalandu akiselebuka.
WAZIRI wa
Mali Asili na Utalii, Lazaro Nyalandu ambaye ametangaza nia ya kuwania
urais wa nchi amefanya kufuru kubwa katika Kanisa la Efatha
linaloongozwa na Nabii Josephat Mwingira, mjini Kibaha, Pwani baada ya
kusakata sebene la Injili usiku wa manane.
Nyalandu ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Singida Kaskazini (CCM),
alifanya hayo juzi katika mkesha wa kuukaribisha mwaka mpya 2015 ambapo
alipanda jukwaani na kusakata muziki huku akishangiliwa na waumini wa
kanisa hilo.
Kuonesha msisitizo, Nabii Mwingira naye aliingilia jukwaani na kucheza
muziki huo wa Injili huku akighani maneno ya Mungu kwa kutumia kipaza
sauti alichokuwa nacho mkononi saa zote za hafla hiyo.
Mara baada ya saa sita na dakika 35 usiku kutimia Nyalandu ambaye
alikuwa mgeni rasmi alikaribishwa kusema neno ambapo alipanda jukwaani
na kumshukuru Mungu kwa kuuona mwaka mpya 2015.
Hata hivyo, alijipigia
kampeni kwa kuwakumbusha waumini hao kuwa Oktoba mwaka huu Tanzania
itakuwa na tukio kubwa, hivyo waumini hao kwake ni muhimu kwani wakati
ukifika atawaomba kura zao.
“Wakati nacheza pale
nimewaona wanakwaya na kuhisi kwamba wana kitu moyoni. Nawaambia Oktoba
ikifika lazima mchague vijana nami nitawahitaji sana kuja kuniimbia,”
alisema.
Waziri wa Mali Asili na Utalii, Lazaro Nyalandu akiwa na viongozi wa kanisa.
Naye Nabii Mwingira alisema mwaka 2015 anatamka wale wote ambao wapo
kanisani hapo na wana dhamira moyoni mwao, watatimiziwa na Mungu wa
Efatha.
“Huwa sisi hatuamini katika mashetani, tunaamini katika roho saba...
hivyo natamka kwamba wote waliopo hapa na wana nia zao katika vifua
vyao, basi Mungu atawapa,” alisema Mwingira huku akishangiliwa.
Hii ni mara ya pili kwa
Nyalandu kujipigia kampeni za urais kanisani, mara ya kwanza ni hivi
karibuni katika jimbo lake alipokwenda katika Kanisa la Kiinjili la
Kilutheri Tanzania kijijini Ilongelo, Singida.
Kiongozi huyo pia alikwenda katika Shule ya Msikiti wa Ilongelo ambapo inadaiwa alitoa msaada wa kusaidia shule na kanisa hilo.
Waziri wa Mali Asili na Utalii, Lazaro Nyalandu.
Hata hivyo, baadhi ya wadau wa siasa waliozungumza na gazeti hili juzi
jijini Dar walisema kuwa anachofanya Nyalandu ni kinyume na maadili ya
chama chake ambacho kinakataza kutumia makanisa na misikiti kujipigia
debe katika mambo ya siasa.
Katibu wa Itikadi na
Uenezi wa Taifa wa CCM, Nape Nnauye hakupatikana ili aweze kutoa maoni
yake kuhusu vitendo hivyo kwani simu yake ilikuwa haipatikani.
Baadhi ya wagombea
waliotangaza nia kutoka CCM ni Dk Hamisi Kigwangalla, Januari Makamba,
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na wengine wanaotajwatajwa ni Steven Wassira,
Bernard Membe, Samwel Sitta na Edward Lowassa.
