
Mbunge wa Monduli (CCM), Edward Lowassa, amesema watu wanaosema anawalipa watu wanaomshawishi awanie nafasi ya urais kwenye uchaguzi mkuu ujao, ni upuuzi na uongo na kwamba hawezi kuwajibu kwani kufanya hivyo ni kuwapa sifa wasizostahili.
Lowassa
aliyasema hayo nyumbani kwake jana mjini Dodoma, kufuatia baadhi ya
vyombo vya habari, kumnukuu Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia, January Makamba, ambaye ametangaza nia ya kuwania urais,
akisema baadhi ya watu wanatumia vibaya umaskini wa Watanzania kwa
kuwakusanya na kuwapa fedha ili waseme wanawashawishi wawanie urais.
Akizungumza
mbele ya wachungaji 110 wa makanisa ya Kipentekoste kutoka sehemu
mbalimbali nchini jana, Lowassa alisema hana uwezo wala sababu ya
kuwagharimia watu wanaofika nyumbani kwake kumshawishi na kwamba wengi
wanafanya hivyo kwa mapenzi yao na Mungu wao.
“Najiunga
na mwenzangu (Mwenyekiti wa CCM Shinyanga, Khamis Mgeja) kusema leo
(jana) kuna mtu kwenye magazeti amesema maneno ya hovyo hovyo kidogo,
ambaye nikimjibu nitakuwa nampa heshima kwa hiyo nampuuza, sina uwezo wa
kuwagharamia watu wote hawa waje nyumbani kwangu na wala sina sababu,” alisema.
Alisema
makundi yanayomshawishi awanie nafasi hiyo wanafanya hivyo kwa utashi
wao, mapenzi yao kwa taifa na Mungu wao na kwamba ‘lugha nyingine
tofauti ni upuuzi tu na uongo.’
Awali,
Mgeja alisema watu wanaosema kuwa wanaofika nyumbani kwa Lowassa
wanalipwa, ni walioishiwa hoja, wamefilisika na sasa wanatapatapa na
kwamba kuwajibu watu hao ni kuwapa sifa wasizostahili kwani baadhi yao
wanahitaji muda mrefu wa kujifunza siasa.
“Nimekaa
muda mrefu kwenye siasa, wengine bado wanahitaji wapate muda wa
kujifunza na katika siasa hatuwajui ni wapi walipotokea, wakipata muda
mzuri wajifunze, wawe na adabu, watulie kuliko kuzusha maneno ambayo
huna uhakika nayo, ambayo ni dhambi kubwa sana,” alisema Mgeja.
Alisema
wakati wa sherehe za miaka 38 ya CCM mkoani Ruvuma, Mwenyekiti wa chama
hicho, Rais Jakaya Kikwete alitoa rai kuomba wananchi na wana CCM
wakiona mtu anayefaa kuwa kiongozi wamshawishi, hivyo wanachokifanya
siyo makosa.
“Tusihukumiane
kwenye hili, Mgeja na wengine wamefika nyumbani kumshawishi, ndivyo
tulivyoombwa kwamba tukiona ana uwezo tumshawishi, mpeni nguvu, mjengeni
suala hili ni kubwa linahitaji dua na maombi. Kama viongozi tumeona kwa
maana tunafahamiana, nani anafaa kupokea kijiti na kutupeleka mbele,
niungane na Watanzania wenzangu na mimi kusema tunaona kwamba hakuna
mwingine zaidi ila Mheshimiwa Lowasa,” alisema Mgeja.
Aidha,
Lowassa alizungumzia ujio wa wachungaji hao nyumbani kwake jana,
akieleza kuwa umeandika historia katika maisha yake kwani hakutegemea
kupokea kundi kubwa kama hilo la watumishi wa Mungu.
Alisema watu ambao wamemfuata kumshawishi amewaambia kuwa nafasi ya urais ni kubwa na inahitaji maombi.
“Ninachoomba
wachungaji mmekuja nawashukuruni sana, mkapige magoti mpaka yachubuke,
hatimaye niweze kusema nayaweza yote katika yeye anitiaye nguvu,” alisema.
Mapema,
Mratibu wa ujio wa Wachungaji hao, Mchungaji Benedickto Kamzee, kutoka
Kanisa la Glory of Christ la Katavi, alisema wamefikia uamuzi huo bila
kushinikizwa wala kushawishiwa na mtu yeyote.
“Hakuna aliyetushawishi, hata siyo maaskofu wetu, hili suala halina msukumo wowote zaidi ya msukumo wa Mungu,” alisema.
Kamzee alisema wachungaji hao wanatoka kwenye madhehebu ya EAGT, TAG, PEFA na KLPT kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Wachungaji hao waliingia nyumbani kwa Lowassa wakiwa na mabango yaliyoonyesha maeneo waliyotoka.
Maeneo
hayo ni pamoja na Meatu, Makete, Karatu, Busega, Bariadi, Bukombe,
Igunga, Chakechake, Mafia, Karagwe, Nachingwea, Temeke, Kinondoni,
Rombo, Monduli, Kilwa, Mkuranga Kasulu na Bunda.
Wengine
wanatoka Handeni, Ngara, Iramba, Mpanda, Bagamoyo, Same, Masasi,
Kibondo, Kilombero, Rungwe, Mwibara, Kisarawe, Nachingwea na Kilolo.
Wanafunzi,Wafanyabiashara wanena.
Wakati
huo huo, wanafunzi wa vyuo vikuu na wafanyabiashara mjini Dodoma
waliokwenda kwa Lowassa juzi kumshawishi agombee, wamesema kwa Lowassa
hakukuwa na ubwabwa wala soda na kwamba kauli ya Makamba inaonyesha kuwa
Lowassa ni kiongozi anayefaa ndio maana watu wanampinga.
Rais
wa Kitivo cha Imformative katika Chuo Kikuu cha Dodoma, Goodluck
Philip, alisema wanafunzi walikwenda kwa Lowassa kwa utashi binafsi na
bila shinikizo na kwamba kauli ya kuhongwa imewadhalilisha.
Alisema kauli hizo zinalenga kuwatisha watu wakati msingi wa kufanya hivyo ni wa kidemokrasia.
Naye
mwenyekiti wa wafanyabiashara mjini Dodoma, Norbati Pangaselo, alisema
wapinzani wa Lowassa wanatakiwa kujenga hoja badala ya kuzusha uongo kwa
nia ya kumchafua.
CREDIT; Mpekuzi blog