
HALI ya huzuni imetawala wakati wa kuagwa kwa aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina Kombani.
Mwili
wa Kombani umeagwa rasmi leo katika Uwanja wa Karimjee jijini Dar es
Salaam tayari kwa ajili ya mazishi kesho mkoani Morogoro.
Watumishi
wa serikali, wana familia ya Kombani na wananchi kwa ujumla
walibubujikwa na machozi wakati wasifu wa kiongozi huyo wa nchi
ukitolewa.
Celina
Kombani ambaye amekuwa mbunge kwa miaka 10 katika Jimbo la Ulanga
Mashariki, mkoani Morogoro alifariki dunia Septemba 23, 2015 katika
Hospitali ya Apolo, India alipokwenda kwa matibabu ya maradhi ya
Saratani yaliyokuwa yakimsumbua kwa muda mrefu.
Baadhi
ya viongozi waliohudhuria tukio hilo ni pamoja na Makamu wa Rais,
Gharib Bilal; Spika wa Bunge, Anna Makinda; Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi
Ombeni Sefue; Makamu Mwenyekiti wa CCM- Bara, Philip Mangula; Mama
Maria Nyerere, Jaji Joseph Warioba pamoja na mawaziri na wabunge
wanaomaliza muda wao.
Salamu
za pole zilitolewa kutoka kwa watu mbalimbali. Salamu kutoka CCM
zilitolewa na Zakia Meghi ambaye amesema, amekuwa akishiriki katika
uandaaji wa Ilani ya uchaguzi ya chama hicho pamoja na kukitumikia
katika nyadhifa mbalimbali.
Kwa
niaba ya umoja wa wabunge wanawake salamu zilitolewa na Angela Kairuki
huku Spika Makinda akitoa salamu kwa niaba ya Bunge huku Makamu wa Pili
wa Rais, Zanzibar Seif Idd akitoa salamu za pole kwa niaba ya Serikali
ya SMZ.
Kombani
alizaliwa Juni 19, 1959 huku akipata elimu yake ya msingi katika Shule
ya Msingi Kwiro (1975), elimu ya sekondari katika shule ya Kilakala
(1978) na ya Kidato cha Tano na Sita katika Shule ya Sekondari ya
Wasichana ya Tabora (1981).
Kombani
alisoma katika Chuo Kikuu cha Mzumbe, Morogoro akibobea katika Utawala
wa Umma. Alitunukiwa shahada ya kwanza mwaka 1985 na baadaye shahada ya
uzamili 1995.
Baadhi
ya nafasi ambazo Kombani aliwahi kuzishika ndani ya CCM ni uenyekiti wa
Umoja Wanawake (UWT) Wilaya ya Morogoro (2002-2005), Mjumbe wa Kamati
ya Utekelezaji CCM Wilaya ya Kilosa (1987-1992).
Kwa
upande wa serikali, Kombani aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Ofisi ya
Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI (2006-2008)
kabla ya kupandishwa ngazi na kuwa waziri kamili wa wizara hiyo hiyo
mwaka (2008-2010).
Baada
ya uchaguzi mkuu 2010 Kombani huyu aliteuliwa kuwa Waziri wa Katiba na
Sheria kabla ya kubadlisha ofisi hiyo mwaka 2014 na kuwa Waziri Ofisi ya
Rais Menejimenti na Utumishi wa Umma, nafasi ambayo aliitumikia mpaka
mauti yalipomkuta.
Viongozi waandamizi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Makamu wa Rais Dr. Bilal akitoa heshima za Mwisho
Mama wa Taifa Mama Maria Nyerere akitoa heshima za Mwisho
Mke wa Rais wa JMT Mama Salma Kikwete akitoa salam za Mwisho
Spika wa Bunge la JMT, Mama Anne Makinda akitoa heshima za Mwisho
Makamu wa Rais Dr. Bilal akitoa salam za pole kwa Mgane wa Marehem
Mpekuzi blog