
Usiku wa August 9 2016 mchezo wa fainali ya UEFA Super Cup ulichezwa katika uwanja wa Lerkendal Norway, kwa kawaida huu ni mchezo ambao unamkutanisha Bingwa wa michuano ya klabu Bingwa Ulaya na Bingwa wa michuano ya UEFA Europa League, hivyo August 9 ilikuwa ni siku ya Real Madrid kukutana na Mabingwa wa Europa Sevilla.

Kwa upande wa Real Madrid wao waliingia uwanjani bila ya uwepo wa staa wao Cristiano Ronaldo ambaye bado anaendelea kuuguza jeraha lake la goti, kukosekana kwa Ronaldo hakukuwa pigo sana kwani Real Madrid walifanikiwa kuibuka na ushindi wa goli 3-2 ndani ya dakika 120, hiyo inatokana na dakika 90 kumalizika kwa sare 2-2.

Mchezo haukuwa rahisi kwa Real Madrid kwani mashabiki wao walikata tamaa kutokana na mchezo hadi dakika ya 89 walikuwa nyuma kwa goli 2-1 ila dakika ya 90 Sergio Ramos akaisawazishia Real, licha ya Real Madrid kuanza kupata goli dakika ya 21 kupitia kwa Marco Asensio.
