Zlatan Ibrahimovic amecheza kwa mara ya kwanza kwenye dimba la Old
Trafford akiwa kama mchezaji wa Manchester United walipocheza na Everton
katika mchezo maalum kwa ajili ya Wayne Rooney ulioisha bila kufungana.
Mshambuliaji wa England Rooney (30), alicheza dakika 52 kabla ya
kutolewa nje na mchezo kusimama kwaajili ya kupigiwa makofi na mashabiki
takriban 58,597 waliohudhuria uwanjani hapo.
Zlatan, ambaye amejiunga na Man United mwezi July alitolewa dakika ya 65.
Beki mwenye asili ya Ivory Coast Eric Bailly ambaye alinunuliwa kwa
paundi mil 30 kutoka Villarreal, pia alicheza kwa mara ya kwanza katika
dimba la OT.
“Usiku wa leo ni usiku ambao mimi na familia yangu tutaukumbuka sana,” Rooney alisema baada ya mchezo kumalizika.
Kocha wa zamani wa Manchester United Sir Alex Ferguson, ambaye
alimsajili Rooney Agosti 31, 2004, na David Moyes ambaye alimfundisha
Rooney kwenye klabu zote mbili walikuwepo.
Zaidi ya hapo, kocha mpya wa England Sam Allardyse pia alikuwepo
katika dimba la OT kumshuhudia Rooney, ambaye amefunga magoli 53 kwenye
michezo 115 kwa taifa lake.
Rooney akiwekewa gwaride maalum kuanzia karibu na eneo la kuelekea
kwenye vyumba vya kubadilishia nguo akiwa na wanawe watatu Kai mwenye
miaka sita, Klay mwenye miaka 3 na Rooney mdogo mwenye umri wa miezi
saba ambao walikuwa wamekaa mahali anapokaa Sir Alex Ferguson.
Rooney, ambaye ni mchezaji wa zamani wa Everton amefungia United
magoli 245 kwenye michezo 520 na kwa sasa anashikilia nafasi ya pili kwa
rekodi ya ufungaji ndani ya klabu hiyo.
Rooney ameshinda makombe matano ya EPL katika kipindi chote
alichodumu klabuni hapo, taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya, kombe moja la
FA, na Fifa Club World Cup.
Pia atakuwa akijaribu kuchukua Ngao ya Jamii kwa mara ya nne wakati
timu yake itakapovaana na Leicester City kwenye dimba la Wembley
Jumapili ijao.
Rooney ametangaza kwamba mapato yote yaliyotokana na mchezo huo
yataenda moja kwa moja kwa watoto na vijana wasiojiweza nchini
Uingereza.