Siku chache baada ya kusambaa kwa sauti katika mitandao ya kijamii,
ikiwemo WhatApp na Facebook, inayodaiwa kutengenezwa kwa lengo la
kumchafua Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe na
mrembo wa Tanzania mwaka 2006, Wema Sepetu, hatimaye ‘dude’ limeamka na
sasa kimenuka.
HAPA NDIPO ILIPOANZIA
Mwishoni mwa wiki iliyopita, sauti iliyorekodiwa kama ya watu wanaoongea
kwenye simu, zilianza kusambaa kwa kasi mitandaoni, ambazo kwa
kuzisikia harakaharaka, zilionekana kufanana na watu hao wawili,
zikisikika kama za watu waliokuwa katika uhusiano.
Wakati sauti hizo zinasambaa, muda mchache baadaye, majibizano ya meseji
kwenye simu yakaanza kusambaa pia, ambayo nayo yanahisiwa kuwa
yalitengenezwa, yakiwahusisha viongozi wawili wa ngazi za juu katika
Mikoa ya Arusha na Dar es Salaam, wakipongezana kwa kukamilika vizuri
kwa kazi hiyo (ya kutenegeneza na kusambaza sauti). Katika majibizano
hayo ya meseji za simu, ‘viongozi’ hao wawili walimsifu mtu waliyemwita
Steve (anadhaniwa kuwa Steve Nyerere) kwa kuifanya kazi hiyo vizuri (ya
kuigiza sauti ya kiongozi huyo).
RISASI LAWASAKA WAHUSIKA
Ili kupata mkanda kamili wa ishu hiyo, Risasi Mchanganyiko liliingia
mtaani na kuifanyia kazi ili liweze kuwapa wasomaji wake kitu cha
kueleweka. Freeman Alkael Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema
Taifa, hakupokea simu aliyopigiwa, lakini wakati Risasi Mchanganyiko
likienda mitamboni, alisikika kupitia kituo kimoja cha redio jijini
Arusha, akiikana sauti hiyo na kusisitiza kuwa hajawahi kuwa na uhusiano
wa kimapenzi na muigizaji huyo na kwamba kinachofanyika ni siasa chafu,
kitu ambacho kitashughulikiwa na chama.
Wema Sepetu naye simu yake iliita bila kupokelewa na hata baada ya
kutumiwa ujumbe mfupi, hakujibu licha ya kuonekana kuwa umepokelewa na
kusomwa.
HUYU HAPA MLEZI WA WEMA CHADEMA
Hata hivyo, Risasi Mchanganyiko lilifanikiwa kumpata mtu aliyepewa
jukumu la kumlea Wema ndani ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), Boniphace Jacob ambaye pia ni Meya wa Ubungo jijini Dar es
Salaam na hapa anafunguka kuhusu ishu hiyo; “Tumeshaongea na wanasheria
juu ya hatua kali za kisheria, kuwachukulia hatua
wote wanaoigiza sauti za viongozi wetu na kuzitumia vibaya kwa nia ya
kuwadhalilisha na kuwashushia heshima, pamoja na kutoa taarifa kwenye
vyombo vya dola juu ya uchunguzi ufanyike kubaini sehemu na watu
wanaofanya “voice studio” kwa lengo ovu.
“Pili tumemtia moyo kamanda wetu Wema kuwa asihofu na siasa za majitaka
na kwamba yote yanafanyika na wapinzani wetu, kwa sababu wanamuhofia na
kumuogopa
juu ya namna anavyofanya mikakati ya kufuta
“UTUMWA WA WASANII KWA CCM”
kazi ambayo ameifanya na mpaka sasa ameandaa ujio wa wasanii wakubwa 20 ndiyo maana wanataka kumuondoa nje ya agenda yake.”
STEVE NYERERE NAYE AFUNGUKA
Steve Nyerere ambaye kwa mujibu wa meseji zilizoenezwa mtandaoni
alionekana kama ndiye aliyeshughulika kutengeneza sauti hiyo ya kiume,
aliruka kimanga kuhusika na suala hilo, aliloliita la kijinga na
kipumbavu. “Mimi sihusiki, sikutengeneza ile sauti kwa vile sina sababu
ya kufanya hivyo,
hicho ndicho ninachoweza kukuambia ila kwa nyongeza tu, niwatake
Watanzania waachane na kufuatilia mambo ya kijinga na kipumbavu, tuna
vitu vingi sana vya kufanya badala ya kukuza vitu kama hivi.”
SASHA NAYE AZUNGUMZIA ‘SAUTI YAKE’
Sasha, msanii ambaye hutumika kama video queen kwenye nyimbo mbalimbali za Bongo Fleva, ambaye
amefanana sauti kwa kiasi kikubwa na Wema Sepetu, anahusishwa kutumika
kutengeneza sauti ya kumuigiza malkia huyo wa filamu Bongo. “Nimetumika
kuiga sauti ya Wema? Hapana, sijawahi kupigiwa simu na mtu yeyote na
wala sijafanya kitu kama hicho, nikuambie ukweli kuwa hili jambo ndiyo
kwanza wewe unaniambia, sijui kabisa,” alisema msanii huyo.
TUNDU LISU ABEZA
Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lisu ambaye pia ni Mbunge wa Singida
Mashariki, alipotakiwa kulizungumzia suala hilo, alisema ni propaganda
dhaifu, zilizolenga kumchafua mwenyekiti wao, ambayo imeshindwa. “Lengo
lao lilikuwa ni kumchafua mwenyekiti wetu, lakini hawajaweza kwa sababu
hawezi kuchafuka kwa staili hii. Tunajua hili jambo hata tukilipeleka
polisi ni kama kujisumbua tu, hawana historia ya kushughulikia shida za
wapinzani.”
HAWA HAPA POLISI MAKOSA YA MTANDAO.
Risasi Mchanganyiko lilimpata mmoja wa maofisa wa kitengo cha makosa ya
mtandao, ambaye alijitambulisha kwa jina moja la Fadhil, akisema yeye
siyo msemaji wa suala hilo. “Ila ninachoweza kukusaidia kwa hili ni
kwamba Cyber Crime haifanyi kazi pasipo kupokea malalamiko. Hao ambao
sauti zao unasema zimeigwa, wanatakiwa waje kulalamika hapa na hapo
ndipo polisi watakapoanza kufuatilia suala hilo. “Lakini kama wenyewe
watakaa kimya bila kulalamika, basi suala hilo litaishia kama lilivyo,
endapo watakuja suala hilo litafanyiwa kazi mara moja,” alisema