VISA VYA CORONA TANZANIA VYAONGEZEKA KUFIKIA 147

Tanzania imethibitisha visa vipya 53 vya ugonjwa wa corona nchini humo hatua inayoongeza idadi ya watu walioathirika na ugonjwa huo kufikia watu 147.

Katika taarifa iliotumwa kwa vyombo vya habari , waziri wa Afya Ummi Mwalimu amesema kwamba wagonjwa wote ni raia wa Tanzania.

Idadi hiyo ni kubwa zaidi kutangazwa kwa siku moja katika taifa la Afrika mashariki tangu wagonjwa wa kwanza wa virusi hivyo kugunduliwa katika eneo hili.

Amesema kwamba miongoni mwa wagonjwa hao 38 wanatoka katika mkoa wa Dar es salaam, 10 katika Kisiwa cha Zanzibar , mmoja kutoka Kilimanjaro , 1 kutoka Mwanza , Pwani Mtu 1 na Kagera mtu 1. 

''Munaweza kuona nimetoa takwimu kubwa sana lakini tumeamua tuseme ukweli kwa sababu Watanzania sasa lazima waelewe kuwa tunakabiliwa na changamoto kubwa." alisema waziri huyo.

Ameongezea kwamba Idadi ya watu waliopona ni 11 huku waliofariki wakiwa 5.

Vilevile amewataka Watanzania kuchukua tahadhari kubwa kujilinda dhidi ya ugonjwa wa Corona.
"Kama kuna mmoja alikuwa na shauku basi ni wakati afahamu Corona inaanza na wewe kujikinga na pia uwakinge wengine" 

Aidha afisa huyo wa serikali amesema kwamba kuna watu wenye dalili za ugonjwa wa corona ambao wamekuwa wakienda kupata huduma za matibabu katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Kutokana na hilo ametoa wito kwa hospitali hiyo kutopokea wagonjwa kama hao akisema kwamba Muhimbili ni hospitali kuu ya rufaa inayokabiliana na magonjwa mengine na badala yake akawataka wagonjwa hao kuripoti katika hospitali ya rufaa ya mkoa ya Amana mjini Dar es Salaam. 

Idadi hiyo ni kubwa zaidi kutangazwa kwa siku moja katika taifa la Afrika mashariki tangu wagonjwa wa kwanza wa virusi hivyo kugunduliwa katika eneo hili.